Saturday, February 9, 2013

Mitaala yamtesa Waziri Kawambwa

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya ufundi Mh. Shukuru Kawambwa
  • MBATIA ATOA KASORO NNE KUPINGA ILE ILIYOLETWA BUNGENI
HOJA binafsi ya mbunge wa kuteuliwa na Rais, James Mbatia, aliyeibana serikali kutaka ilete bungeni nakala ya mitaaala ya elimu nchini, imezidi kumweka pabaya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa. Nakala ya mitaala hiyo ambayo imezua mjadala ndani na nje ya Bunge kwa wiki nzima sasa, ilikabidhiwa kwa wabunge jana na kuibua mzozo mpya.

Mara baada ya Spika Makinda kugawa nakala hizo na kulieleza Bunge kuwa mitaala hiyo ni halali, Mbatia alikuja juu kuomba mwongozo wa Spika kupinga uhalali wake. Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, aliainisha kasoro nne kuonyesha kwamba mitaala hiyo imechakachuliwa.

  1.  Alisema aliomba kuletewa nakala ya mitaala ya elimu ya kutoka mwaka 1977 hadi 2005, lakini nakala ya mitaala iliyoletwa bungeni ni ya mwaka 1978 hadi 2005.
  2. Pili alisema mitaala iliyoletwa bungeni imechakachuliwa kwani haina ISB namba inayotolewa na Bodi ya Maktaba Nchini.
  3. “Tatu, alisema mitaala hiyo haina saini ya Kamishna wa Elimu Nchini kwani lazima asaini kuonyesha mitaala hiyo ni halali na ni mali ya serikali. “Ukiangalia kwenye muhtasari huu wa elimu nilioushika hapa, kuna ISB namba inayotolewa na Bodi ya Maktaba na imesainiwa na Kamishna wa Elimu. Hii mitaala lazima pia isainiwe na Kamishna wa Elimu na iwe na ISB, lakini hii haina,” alisema Mbatia.
  4. Kubwa kuliko yote, Mbatia alisema mitaala ya elimu inapaswa kuwa ya Tanzania nzima, lakini hii iliyoletwa bungeni imeandikwa kwa ajili ya Tanzania Bara tu, jambo ambalo sio sahihi. Katika mwongozo huo ambao haujatolewa uamuzi, Mbatia aliliomba Bunge lijadili mitaala hiyo kubaini kama ni sahihi.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi huo wa Bunge, alisema serikali imeshindwa kuleta kile alichokitaka hivyo hawezi kujiuzulu.

Naye Waziri Kawambwa alipozungumza na wanahabari nje ya ukumbi wa Bunge, alisema kuna makosa ya uchapaji ndio maana mitaala hiyo imeandikwa kutoka mwaka 1978 hadi 2005 badala ya 1977 hadi 2005.
Kuhusu saini ya Kamishna wa Elimu, alikiri kuwa kweli haina saini yake lakini ameandikia hati kuonyesha uhalali wa mitaala hiyo. Waziri Kawambwa alikiri kuwapo kwa kosa lingine la uchapaji linaloonyesha mitaala hiyo ni kwa ajili ya Tanzania Bara wakati ilipaswa kusomeka kuwa kuwa ni kwa ajili ya Tanzania nzima. Alisema pamoja na kasoro hizo za uchapaji, mitaala hiyo ni halisi na ndiyo inayotumika kwa sasa.

Mmoja wa wajumbe wa tume iliyoundwa kuchunguza uhalali wa mitaala hiyo, Mchungaji Israel Natse, alisema kulikuwa na ubishani mkubwa kwenye kamati kuhusu kasoro hizo. “Kibaya zaidi tulipewa hadidu za rejea moja tu inayosema tuangalie uhalali wa mitaala hiyo. Hivyo hatukuwa na wigo mpana kuchambua kasoro hizo,” alisema.
Awali akikabidhi nakala hizo, Spika wa Bunge Anne Makinda alisema Bunge liliunda kamati ya wabunge sita kuthibitisha mitaala hiyo kama ni halali au la. “Napenda kuwaarifu wabunge kuwa kamati hiyo imemaliza kazi yake na nyaraka hizo ni halali na sasa nazigawa kwenu,” alisema.

Timu hiyo iliundwa juzi na Naibu Spika, Job Ndugai, kupitia nakala hizo ili kubaini kama ni halisi au la kabla ya kukabidhiwa kwa wabunge. Mwenyekiti wa tume hiyo ni Magreth Sitta na wajumbe wake ni Bernadetha Mshashu, Jabir Malombo, Khalifa Khalifa, Mchungaji Israel Natse na Yahya Kassim Issa

Tanzania Daima


0 Maoni:

Post a Comment