MICHEZO

KAMATI ya Uchaguzi Klabu ya Yanga imesema inakerwa na tabia ya Baraza la Wazee la Yanga kuingilia kati masuala ya uchaguzi na kulitaka kukaa pembeni na kuipa fursa kamati husika kufanya kazi hiyo.

Sambamba na kauli hiyo, wagombea watatu wa uchaguzi wa klabu hiyo baadaye mwezi ujao, wamewekewa pingamizi, huku pia zoezi la usaili likipelekwa mbele mpaka Juni 22.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, John Mkwawa alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, kamati yake ni huru hivyo haipaswi kuingiliwa na mtu au kikundi chochote.

Mkwawa alisema kamati yake ina mamlaka ya kumchukulia hatua mtu yeyote atakayekwenda kinyume na taratibu za uchaguzi ambazo wao ndiyo wenye jukumu la kusimamia.

Kauli hiyo ya Mkwawa imekuja siku moja baada ya mwanzoni mwa wiki hii baraza hilo ya Yanga kutishia kumfukuza uanachama  Ahmed Falcon.

Falcon alitishiwa kufukuzwa uanachama kufuatia uamuzi wake wa kuiwekea pingamizi katiba ya Yanga pamoja na wagombea wote wa uchaguzi huo.

Katika madai yake, Falcon alisema katiba inayotumika kwenye uchaguzi huo ni batili kwa vile ina upungufu, jambo ambalo lilipingwa na wazee.

Lakini kwa upande wake, Mkwawa aliwataka wale wote waliowawekea pingamizi wagombea kwenye uchaguzi huo kuwasilisha vithibitisho leo Makao Makuu ya Klabu.

Wagombea waliowekewa pingamizi ni pamoja na mfanyabiashara maarufu nchini, Ally Mayayi na Stanley Kevela.

Aidha, Mkwawa amesema kamati yake imetupilia mbali pingamizi la mwanachama Falcon kwa madai kuwa halina msingi.

Mkwawa alisema madai ya Falcon hayana mashiko na yameshindwa kuwashawishi kukubaliana naye kwa vile katiba itakayotumika kwenye uchaguzi huo inatambulika kisheria.

"Katiba inayotumika ni mwaka 2010, inatambulika kisheria na imepitishwa na Msajili wa Vyama vya Michezo na kukubaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)," alisema Mkwawa.

Ikumbukwe pia kuwa, baraza hilo la wazee Yanga ndilo lililokuwa chemchem ya vuguvugu la mageuzi ya kutaka mabadiliko ya uongozi kwenye klabu hiyo.

Wazee hao walianza kwa kutaka kukabidhiwa timu siku chache kabla ya Yanga kupambana na Simba katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu, ambao Yanga walifungwa mabao 5-0.Hata hivyo madai yao yalipingwa na uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti Llyod Nchunga na baada ya siku chache wakaanzisha shinikizo la kutaka mwenyekiti wao kuachia ngazi.
Katika kutimiza matakwa yao, baraza hilo la wazee liliitisha mkutano wa wanachama uliofanyika Makao Makuu ya Klabu hiyo lakini bila baraka za uongozi na kutangaza kumtimua Nchunga.
Hata hivyo, mapinduzi hayo yalipingwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kabla ya Mwenyekiti Nchunga kukubalia kuachia ngazi baada ya shinikizo la kumtaka kuachia ngazi kukolea.