BURUDANI

Kidumu, Msechu kupamba Miss University Arusha

Peter Msechu
 
Msanii kutoka nchini Burundi, Jean Pierre maarufu kama Kidum na nyota wa bongofleva, Peter Msechu, wanatarajia kuburudisha wananchi wa mkoa wa Arusha na vitongoji vyake katika shindano la kumsaka mrembo wa vyuo vikuu vya mkoani, Redd's Miss University Arusha hapa shindano linatarajiwa kufanyika Jumamosi.

Akiongea na wana habari jijini hapa, mwandaaji wa shindano hilo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fame City Decor, Gaudencia Magessa alisema Diamond na Kidum watatumbuiza kwenye ukumbi wa Naura wakati wa shindano hilo.

Alibainisha kuwa warembo 14 kutoka katika vyuo mbalimbali vilivyopo jijini hapa wanatarajiwa kupanda stejini kuwania taji hilo. Miongoni mwa vyuo wanavyotoka warembo hao ni Chuo cha Uhasibu Arusha, Chuo Kikuu cha Makumira na vyuo vingine.

Alitaja zawadi zitakazotolewa kwa washindi kuwa ni Sh. 500,000 kwa mshindi wa kwanza, Sh. 300,000 kwa mshindi wa pili na Sh. 200,000 kwa mshindi wa tatu.

Alisema lengo la mashindano hayo ni kumpata mrembo wa vyuo vya Arusha na pia kupata fedha za kusaidia jamii mbalimbali za mkoani hapa ikiwa ni pamoja vituo vya kulelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.

"Tutalipia ada pia watoto yatima na wasiojiweza ambao wanahitaji kusoma lakini hawana uwezo. Na huu  ni mwanzo tu, tutaendelea kufanya hivi kila mara," alisema Gaudencia.

Alitoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi katika shindano hilo kwani mbali na kupata burudani ya aina yake kutoka kwa warembo na nyota hao wa muziki pia watakuwa wamewachangia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Alitaja baadhi ya wadhamini wa shindano hilo kuwa ni kampuni ya bia ya TBL kupitia kinywaji chao cha Redds, Real Metal Graft, Modern Supermarket, Perfect Supermarket, SG Resort, Mwandago Investment, Libeneke La Kaskazini blog, Mount Meru Pure Drinking Water na Kasse Store.

Wakati huo huo, kituo cha kulelea watoto yatima cha Hope Orphans kimetoa shukurani kwa waandaaji wa shindano hilo kwa kuwapelekea msaada wa vyakula.

Akizungumza wakati akipokea msaada huo mwakilishi wa kituo hicho,  Lucy Juma, alisema kuwa wanashukuru msaada huo kutoka kwa warembo hao kwani utawasaidia katika kipindi hiki huku akitoa wito kwa wananchi wengine kuendelea kusaidia vituo hivyo.

Akikabidhi msaada huo, Gaudencia Magessa, alisema kuwa wameamua kuwasiadia watoto hawa ili nao wajisikie kama watoto wengine.

Alisema msaada huo umejumuisha mchele, unga wa ugali, mafuta ya kupikia, maji ya kunywa na sabuni.
 
CHANZO: NIPASHE