Spika wa Bunge Mh. Anna Makinda
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimedhamiria kumtumia Spika wa Bunge,
Anne Makinda, kuandaa mkakati wa kuwaumbua na kuwazima kisiasa
wanasiasa kadhaa wa CCM na upinzani wanaosemekana kuwa “wasumbufu”,
wakiwamo Spika aliyepita Samuel Sitta, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe
Zitto, na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.
Katika kutekeleza dhamira hiyo, Makinda anachukua hatua mbalimbali za
kiutawala, zenye lengo la kupunguza makali ya wanasiasa hao,
wanaoonekana kuwa na malengo mapana ya kisiasa mbele ya safari.
Mbali na hilo, Makinda, ambaye pia anasemekana “kuwekwa mfukoni na
serikali” amedhamiria kupunguza nguvu za upinzani kwa ama kutumia kanuni
za Bunge au kuvunja baadhi ya kanuni hizo.
Katika kutekeleza moja ya hatua hizo, jana Makinda alifanya mabadiliko
makubwa ya kamati za Bunge, akafuta baadhi ya misingi iliyoachwa na
Sitta.
Katika kukamilisha mpango huo, Makinda aliunganisha kamati mbili za
Bunge zilizokuwa zinaongozwa na wabunge wa upinzani - Kamati ya Hesabu
za Mashirika ya Umma iliyokuwa chini ya Zitto na Kamati ya Hesabu za
Serikali iliyokuwa chini ya John Cheyo wa UDP.
Maana yake ni kwamba, Zitto na Cheyo watalazimika kupigiwa kura ili apatikane mmoja wa kuongoza kamati mpya.
Baadhi ya wachambuzi wa habari za siasa wanasema kimantiki iliyovunjwa ni kamati ya Zitto, ambayo inaunganishwa na ya Cheyo.
Wanasema lengo ni kumaliza nguvu na machachari ya Zitto, ambaye hana ukaribu na CCM kama alivyo Cheyo.
Mbali ya mkakati huo wa kumkomoa Zitto, Makinda pia ana mkakati wa
kupunguza idadi ya wapinzani katika Kamati ya Uongozi ya Bunge kutoka
watatu hadi wawili.
Wachambuzi wanasema hizi ni jitihada za Makinda kufuta nyayo za Sitta,
kwani ndiye aliyepitisha kanuni zilizowapatia wapinzani kamati tatu, na
kuingiza wajumbe watatu wa upinzani katika kamati ya uongozi.
Makinda hakuishia hapo. Amevunja pia Kamati ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, ambayo pia iliasisiwa na Sitta.
Lakini tafsiri pana ya uamuzi huo ni kwamba, kwa kuivunja kamati hiyo na
kuunda mbili, amemfanya Lowassa aongoze Kamati ya Ulinzi na Usalama,
huku ya nje ikitafutiwa mtu mwingine.
Wajuzi wa siasa za ndani ya CCM wanasema uamuzi huo umelenga kumnusuru
Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambaye
hakuwa anapenda wizara yake kuwekwa chini ya kamati inayoongozwa na
Lowassa.
Ikumbukwe Membe amekuwa akitajwa kuwa hasimu wa kisiasa wa Lowassa ndani ya chama katika kinyang’anyiro cha kuwania urais 2015.
Miezi kadhaa iliyopita, Membe alilalamikia hatua ya kamati ya Lowassa
kutembelea balozi za Tanzania nje ya nchi, hasa Ulaya na Marekani.
Malalamiko hayo yalihisiwa kwamba kuna jambo Membe hakutaka kamati ya
Lowassa ilijue katika balozi zetu; na kwa mantiki hiyo hakutaka
kuwajibika kwake kwa sababu za ushindani wao wa kisiasa.
Mbali na Membe, mtu mwingine ambaye amekuwa hasimu wa kisiasa kwa miaka
ya karibuni ni Sitta, ambaye aliunda kamati iliyofanya uchunguzi wa
sakata la Richmond, ambalo lilimfanya Lowassa ajiuzulu uwaziri mkuu
mwaka 2008.
Kwa kuwa na wizara ya Sitta ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilikuwa
chini ya kamati ya Lowassa, kitendo cha Makinda kuiondoa kwake kinampa
ahueni Sitta, ambaye naye asingependa kusimamiwa na kamati inayoongozwa
na Lowassa.
Baadhi ya wabunge wanaomkosoa Makinda, pamoja na kutambua kuwa anafanya
hivyo kumnusuru Membe na kupalilia sokomoko la kisiasa ndani ya CCM,
wamesema analenga pia kudhoofisha nguvu ya upinzani bungeni.
Wanasema anafanya hivyo ili kujipendekeza kwa serikali na CCM, huku
akilenga kuwania tena uspika 2015, kipindi ambacho tayari ameshatangaza
kuwa hatagombea ubunge.
Miongoni mwa mawaziri ambao wanasemekana kutumiwa na serikali kumdhibiti na kumpotosha Makinda ni William Lukuvi.
Vile vile, wachambuzi wanasema hakuna mantiki ya kuivunja kamati ya
Zitto, yenye kushughulikia mashirika 280, halafu ikaunganishwa na kamati
yenye majukumu mazito kama ya Cheyo.
Wanadai Makinda anakusudia kupunguza makali ya kamati tatu nyeti
zilizokuwa zinatumiwa na wapinzani kuleta uwazi zaidi katika kuisimamia
serikali.
Kamati ya wapinzani ambayo haikuguswa ni ya Hesabu za Serikali za Mitaa
inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP), anayesemekana
kuwa kipenzi cha CCM na Rais Jakaya Kikwete.
Kabla yake, kamati hiyo ilikuwa inaongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA).
Kamati hizi zimekuwa msaada mkubwa sana kwa kusimamia fedha za serikali
kuu na zile za mitaa, lakini kwa mabadiliko yaliyofanywa na Makinda,
wapinzani watabakiwa na fursa finyu.
Kwa siku za karibuni, Zitto ameonekana kuisumbua serikali katika masuala
mbalimbali, na alitoa matamko makali katika sakata la gesi ya Mtwara.
Kijumla huu ni mkakati wa Makinda kuidhibiti CHADEMA bungeni ili
isiongoze kamati nyeti, kwani hata jinsi Mrema na Cheyo walivyopewa
fursa hizo, ilitokana na kupindwa kwa kanuni.
Kimsingi kamati zao zilipaswa kuongozwa na wabunge wa CHADEMA ambao kikanuni ndio wanaunda kambi rasmi ya upinzani bungeni.
Baadhi ya wabunge wanasema huu ni ushahidi mwingine wa ubabe wa Makinda,
kwani kanuni za Bunge hazijabadilishwa ili kumwezesha kuunda na kuvunja
kamati hizi mpya.
0 Maoni:
Post a Comment