Mbunge
wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, ametimuliwa kwenye kikao cha Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kwa madai kwamba
ana maslahi ya upande mmoja katika mgogoro uliotokea bungeni juzi wakati
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, alipokuwa akijibu hoja ya
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.
Taarifa
za uhakika zilizopatikana bungeni jana zilieleza kwamba Mdee ambaye ni
mjumbe wa kamati hiyo, alizuiwa kuhudhuria kikao kilichojadili sakata
hilo kwa kuwa alikuwa akishabikia vurugu bungeni.
Taarifa
zaidi zimedai kwamba kumeibuka mvutano kuhusu kanuni iliyotumika
kumruhusu Waziri Maghembe kutumia nusu saa kujibu hoja ya Mnyika wakati
alipaswa kutumia dakika 15 kama wachangiaji wengine.
Jana
Mdee alithibitishia NIPASHE kuwa alizuiwa kuhudhuria kikao cha kamati
hiyo kwa maelezo kuwa ana maslahi na upande wa kambi ya upinzani juu ya
suala la mgogoro wa hoja ya Mnyika ambayo ilipokwa na serikali juzi na
kuiua.
Mdee
alielezwa kuwa alikuwa bungeni siku hiyo na alishiriki katika kadhia
iliyosababisha Bunge kuahirishwa kabla ya muda wake baada ya wabunge
wote wa Chadema na NCCR-Mageuzi kusimama kwa muda mrefu na kuzuia
shughuli za Bunge kuelendelea wakipinga kitendo cha kuvunjwa kwa kanuni
za Bunge kwa kuipa nafasi serikali uondoa hoja binafsi ya Mnyika juu ya
upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka katika jiji la Dar es
Salaam.
Kamati
ya Maadili imepewa jukumu la kuchunguza chanzo cha vurugu hizo kwa
kuwahoji wabunge waliohusika na kadhia ya Jumatatu jioni ili kutoa
mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa dhidi yao.
WAJUMBE WA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE
Brigedia Jenerali
Hassan Ngwilizi (Mwenyekiti); Christopher Ole Sendeka; Rashid Ali
Abdallah, Dk. Maua Daftari; John Chiligati; Dk. Christina Ishengoma;
Riziki Omar Juma; David Kafulila; Vita Kawawa; Philemon Ndesamburo;
Augustino Masele, Said Arfi; Augustine Mrema; Cynthia Ngoye; Halima Mdee
na Gosbert Blandes.
Hata hivyo,
Chadema imewaelekeza wabunge wake wote kutoitikia wito wa kamati hiyo
hadi hapo Spika wa Bunge, Anne Makinda, atakapotoa uamuzi wa rufaa 10
ambazo wabunge hao wamekata kwake, lakini amezikalia tangu mwaka 2011.
Pia Chadema
kimetishia kuwasilisha hoja ya kumng'oa madarakani Spika Makinda na
Naibu Spika, Job Ndugai, kwa madai ya kukiuka kanuni za Bunge kwa
kutotenda haki kwa pande zote, hasa kambi ya upinzani, kwa maana hiyo
wamepoteza sifa za kuongoza muhimili huo.
WABUNGE HAWAJAHOJIWA
Wakati huo huo, Kamati hiyo bado haijawahoji wabunge wanaodaiwa kufanya fujo ndani ya Bunge.
Taarifa zilizoifikia NIPASHE, zilieleza kwamba hakuna hata mbunge mmoja ambaye amepewa samansi ya kuitwa kwenye kamati hiyo.
Katika hatua
nyingine, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu,
amesema kitendo cha Spika wa Bunge, Anne Makinda, kumtuhumu kuwa ni
mropokaji namba moja bungeni ni kwa sababu ya chuki na upendeleo dhidi
ya wabunge wa upinzani.
Akizungumza na
NIPASHE jana Lissu alisema siyo kweli kwamba amekuwa ni mropokaji
bungeni kama Spika Makinda alivyomtuhumu na kwamba amekuwa akifuata
kanuni zinazotakiwa kwa kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuisimamia
na kuishauri serikali.
Alisema yeye ni miongoni mwa wabunge wachache ambao wanazifahamu kanuni za Bunge, Katiba ya nchi na sheria mbalimbali.
“Kuniita mropokaji
ni kunifananisha na baadhi ya wabunge wa CCM ambao hawajui sheria wala
wajibu wa Bunge…wanadhani kazi ya mbunge ni kuikingia kifua serikali na
kuitetea, wamesahau kwamba wajibu wao ni kuishauri na kusimamia, "
alisema.
Lissu alisema
kamwe hawezi kuogopa kuisimamia serikali kama Katiba inavyomtaka na
hawezi kuitetea pale inaposhindwa kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.
KAMATI KUCHUNGUZA MTAALA
Katika hatua
nyingine, Bunge limeunda kamati ya wabunge sita kuchunguza mitaala ya
shule ya awali, msingi na sekondari iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, ili kubaini kama ina
upungufu au la.
Hatua hiyo imekuja
baada ya Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, wiki
iliyopita, kuitaka serikali kuonyesha mitaala hiyo.
Naibu Spika wa
Bunge, Job Ndugai, alisema baada ya kipindi cha maswali na majibu
bungeni jana kuwa amekabidhiwa mitaala hiyo na ameunda kamati hiyo ili
ikajiridhishe juu ya jambo hilo.
Wajumbe wanaounda
kamati hiyo ni Mbunge wa Kibiti (CCM) Abdul Jabiri Marombwa; Mbunge wa
Chwaka (CCM), Yahya Kassim Issa na Mbunge wa Karatu (Chadema), Israel
Natse.
Wengine ni Mbunge
wa Viti Maalum (CCM), Benardetha Mushashu; Mbunge wa Viti Maalum (CCM)
Margaret Sitta na Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa.
Ndugai alisema
wengine watakaoingia kwenye kamati hiyo kuwa ni Mbatia, Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, Kamishina wa Elimu, Mwanasheria wa Wizara na
wataalamu wengine wa elimu.
Hata hivyo, Ndugai
aliitaka kamati hiyo kufanya kazi yake jana na ifikapo leo iwe imekuja
na majibu juu ya suala hilo. Wiki iliyopita, Mbatia aliwasilisha bungeni
hoja binafsi kuhusu udhaifu katika sekta ya elimu na kutaka mfumo
unaosimamia elimu nchini ufumuliwe.
Alitaja udhaifu
uliopo katika sekta ya elimu kuwa ni pamoja na kutokuwapo sera ya pamoja
kuhusu elimu, matatizo ya mitaala na utungaji wa vitabu vya kufundishia
shuleni.
Hoja ya Mbatia ilizua mjadala mrefu bungeni kuhusu kuundwa kwa kamati ya kuchunguza mitaala, sera na mihutasari ya elimu.
Baadhi ya wabunge walitaka kamati ya Bunge na wengine walitaka iundwe tume huru ya kufuatilia suala hilo.
Mjadala huo
uliendelea kwa Dk. Kawambwa kutetea mfumo wa elimu uliopo na mtaala,
kabla ya wabunge kuchangia na Mbatia kuhitimisha hoja yake.
Akiwasilisha hoja
yake, Mbatia aling’ang’ania kupatiwa mitaala hiyo, jambo ambalo Dk.
Kawambwa alijibu kuwa ilikuwapo ingawa hakuwa nayo bungeni.
Baada ya majibu ya Dk. Kawambwa, Mbatia aliomba hoja yake iahirishwe hadi mitaala itakapowasilishwa bungeni.
Awali, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi,
alisimama bungeni na kuhoji: “Katika kikao kilichopita, hata katika
hansard, tulisema mtaala utawasilishwa katika kikao hiki, sasa wasiwasi
wa mbunge (Mbatia) ni nini? Hata siku ya mwisho ya Bunge tutaleta.”
Baada ya kauli
hiyo, Ndugai alipiga kura kwa kuuliza wanaotaka hoja imalizike na baada
ya majibu, aliruhusu Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Hamisi Kigwangalla,
kuwasilisha hoja binafsi kuhusu ajira kwa vijana na kilimo.
Hata hivyo, baada
ya kumruhusu Dk. Kigwangalla, wabunge wa upinzani walitoka nje ya Bunge
na kufanya mkutano wa dharura uliochukua dakika 38 katika ukumbi wa Pius
Msekwa.
HAKIELIMU YAIBANA SERIKALI
Katika hatua
nyingine, serikali imetakiwa kuacha ubabe wa kupangua hoja zinazotolewa
na watalaamu wa masuala ya elimu, ambao wanafanya utafiti na kuainisha
upungufu uliopo katika sekta hiyo.
Kauli hiyo
ilitolewa jana na wanaharakati wa masuala ya elimu, ambao wameunga mkono
hoja iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni na Mbatia, aliyetaka Bunge
lichunguze udhaifu uliopo katika sekta ya elimu nchini.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la HakiElimu linalojishughulisha na masuala ya
elimu, Elizabeth Misokia, aliwaaambia waandishi wa habari ofisini kwake
jana kuwa Tanzania ni ya Watanzania wote na kwamba, kitendo cha serikali
kukosoa tafiti za watalaamu na kuzitupa, hakilengi kuijenga nchi na
kuinua kiwango cha elimu nchini.
“Serikali isitumie
nguvu nyingi kukosoa tafiti mbalimbali zinazofanywa na watalaamu kuhusu
elimu, badala yake izifanyie kazi ili kuziboresha,” alisema Misokia.
Alisema sera ya
elimu ya mwaka 1995 haieleweki inasema nini kuhusu elimu na kwamba, hata
mitaala ya kufundishia nayo haileweki kwa walimu wanaoitumia
kufundishia.
Misokia alisema
sekta ya elimu nchini inakabiliwa na matatizo mengi, ukiwamo uhaba wa
walimu, walimu kukata tamaa kutokana na serikali kuwapuuza, kushindwa
kuwalipa madai yao ya siku nyingi pamoja na kufanya kazi katika
mazingira magumu.
Matatizo mengine
yanayoikabili sekta ya elimu, ni pamoja na wakaguzi kushindwa kufika
katika shule mbalimbali kwa ajili ya kuzikagua.
Alisema kati ya
mwaka 2000 hadi 2002 elimu ya shule ya msingi ilipanuliwa, lakini hakuna
juhudi zozote za kuwapo sera moja ya elimu itakayoisimamia kikamilifu.
Aliomba serikali
kutengeneza kwanza sera yenye nguvu kuhusu elimu kabla ya kuanza kuandaa
mitaala inayofanana nchini kote ili kuhakikisha wanafunzi wanapata
elimu inayofanana na iliyo bora.
Chanzo: Nipashe | 7th February 2013
0 Maoni:
Post a Comment