Saturday, January 19, 2013

Halima Mdee apandikiza kiburi wananchi wa Chasimba


Mbunge wa Jimbo la Kawe katika Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam, Halima Mdee amewataka wakazi wa Chasimba, Chatembo na Chachui kutoa ushirikiano katika zoezi la uthamini wa maeneo yao yenye mgogoro wa muda mrefu na kiwanda cha saruji cha Wazo Hill.

Mdee aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara na wananchi hao ambao ulifanyikia kwenye viwanja vya Serikali ya Mtaa ya Basihaya iliyopo Chasimba na kuhudhuriwa na madiwani, John Morro wa kata ya Wazo na Sharif  Majisafi wa kata ya Bunju.

Mdee akiwahutubia wananchi hao alisema kuwa licha ya kuwepo na hukumu ya Mahakama ya Rufaa iliyowapa ushindi kiwanda cha saruji cha Wazo Hill dhidi ya wananchi hao, lakini hakuna mwananchi atakayeondoka katika maeneo hayo.

"Kwa kuwa tayari mlishakubaliana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka wakati alipokuja kuhusiana na kuwekwa  mipaka na kufanyika kwa zoezi la uthamini, acha lifanyike ili msionekane ni vikwazo lakini huku kwenye vichwa vyenu mkiwa mnaelewa kuwa hakuna mwananchi atakayetoka hapa maana linafanyika na nyinyi mkiwa humu," alisema Mdee.

Alisema kuwa tathmini ni kutimiza matakwa kisheria kutokana na nchi kuendeshwa kwa sheria, hivyo hakuna sababu ya kulikataa zoezi hilo ambalo linaonyesha serikali kama ina nia nzuri ya kutaka kumaliza mgogoro huo wa muda mrefu kati ya kiwanda cha Wazo na wananchi wa maeneo hayo.

"Serikali inaonekana kama inataka kumaliza mgogoro kati yenu na kiwanda cha Wazo, hivyo tuwape ushirikiano katika zoezi hilo, twende nao lakini tukiona njia tunayokwenda nao si nzuri kila mmoja 'asepe' na njia yake," alisema.

Aliongeza kuwa maeneo hayo kufanyiwa tathimini inaweza kuwa neema kwa wakazi hao kuweza kupata huduma nyingi ikiwemo umeme na maji kwa njia za haki badala ya njia za panya kama ilivyo sasa.

Mdee alisema kuwa nyaraka zilizopo sasa zinaonyesha kuwa maeneo hayo yapo katika eneo la kiwanda, hivyo ili yatengane na eneo la kiwanda ni lazima mipaka iwekwe na tathimini ifanyike.

"Sisi viongozi wenu tupo na nyinyi kwa asilimia mia moja na msimamo wetu ni nyinyi kubaki katika maeneo haya, kama serikali ilifanya uzembe kummilikisha mwekezaji eneo kubwa kwa njia inazojua yenyewe imlipe fidia aondoke nyinyi mbaki na si vinginevyo," alisema.
CHANZO: NIPASHE

0 Maoni:

Post a Comment