Friday, June 15, 2012

Chadema wamefanya makubwa tanzania: Tutarajie mapambazuko zaidi ya kifikra!

Ni kweli chama kinakubalika
Kwa mwendo huu

CHADEMA wanastahili pongezi na kuheshimiwa.

"KAMA watu wawili wana fikra sawa na mtazamo sawa katika kila kitu cha kila jambo, basi, kuwa na uhakika kwamba ni mmojawao tu ndiye mwenye kufikiri”-Lyndon Baines Johnson (LBJ) raisi wa 36 wa Marekani (1963-1969)(Tafsiri).

Ipo mitazamo na imani mbalimbali za kibaguzi iliyojaribu kujengwa dhidi ya vyama vya upinzani toka kuanza kwa mfumo wa vyama vyingi nchini inayolenga kudumaza changamoto za kifikra. Wapo watu wengi walioamini/wanaoamini upinzani ni njama ya kihaini, kashfa, mauaji, matusi, uzushi, au machafuko yanayoondoa dhana halisi ya kichocheo cha changamoto za demokrasia au maendeleo. Wapo baadhi ya viongozi wa kisiasa waliamini/wanaamini kwamba ukubwa wao au mali zao zinastahili kuwalinda hata wanapofanya maovu, hujifikiria wao zaidi na wanaowahusu kuliko manufaa ya taasisi au eneo waliomo na kujidanganya kwa kudhani siku zote watakuwa katika hali na nafasi waliyonayo.

Wakati huu ambapo CHADEMA kinazidi kukubalika kwa kasi kuna baadhi ya watu wanahoji: Je hao CHADEMA wamefanya nini? Ni haki yao ya kimsingi kuhoji lakini naomba niwakumbushe: wamesahau kwamba leo hii kila jambo wanalofanya CCM wanatazama upande wa pili CHADEMA watasema nini?, wanaangalia mbele, wananchi kwa ujumla watasema nini? Nadhani sasa tuweke wigo mpana wa kifikra kutazama nini kazi ya upinzani katika kuleta ushindani wa kisiasa, kudumisha demokrasia, kuimarisha utawala bora na kujenga misingi imara zaidi ya maendeleo?

Kwa nafasi waliyonayo CHADEMA kama chama kikubwa cha upinzani nchini wanastahili sifa na heshima kubwa. Kujenga na kuimarisha chama cha siasa si kazi lelemama, ni kazi inayohitaji UMAKINI, UVUMILIVU na UJASIRI. Kazi kubwa ya chama chochote cha upinzani ni kupima na kupinga ufanisi duni wa serikali ya chama kinachotawala na kujiweka katika nafasi ya kuaminiwa na wananchi ili kupewa ridhaa ya kuongoza na kuongeza ufanisi katika kusukuma gurudumu la maendeleo. Na haya ndio baadhi ya machache ambayo CHADEMA inafanya kama chama cha upinzani Tanzania.Tayari CHADEMA wamefanya na wanafanya, sasa tuwaulize wale wanaosema CHADEMA wamefanya nini walitaka wafanye nini?

Bila ujasiri wa wabunge wachache wa CHADEMA kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 jamii ilikuwa imefunikwa kwenye wingu kubwa la kufungwa kufikra juu ya mustakabali wa nchi yao. Wamesahau kwamba bila CHADEMA leo hii usingesikia wimbo wa kujivua MAGAMBA ndani ya CCM.

CHADEMA wamefungua minyororo ya kifikra na kuleta mapamazuko mapya. Ieleweke kwamba maendeleo yoyote ya kiuchumi na kijamii yanaanza na mapambazuko ya kifikra. "Hakuna jibu moja linaweza kutumika wakati wote na mahali pote","bila kutambua kwa utashi, kuelewa na kukubali juu ya matatizo yetu, hatuwezi kufanya maamuzi sahihi katika kudai haki za kimsingi katika jamii. Dhana ya kufikiri kwa bidii dio nyenzo muhimu ya kulinda uzalendo na uadilifu bila kuathiri utu wetu.
“…kuchaguliwa kuunda utawala wa kuongoza nchi hakumaanishi kuchaguliwa kujitawalia mamlaka ya umma na kisha kutumia mamlaka hayo kuwakandamiza “waliokuchagua” kwa sababu tu ya kutetea maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma”. (Katiba ya CHADEMA)

Uwepo wa CHADEMA haulengi kugawa wananchi katika jamii yetu ili kudhoofisha maendeleo kama baadhi ya watanzania wenzetu wanavyotaka tuamini, bali ni njia ya kulinganisha sera, fikra na mitazamo katika kuchochea maendeleo.

Think Twice...Act and react wise!

0 Maoni:

Post a Comment