Friday, October 26, 2012

Leo ni Eid-el-Adh'haj

Al-Kaaba, jiwe tukufu.

Leo ni sikukuu ya kuchinja kwa waumini wa Kiislamu ulimwenguni kote, ambapo wanasherekea baada ya mahujaj kukamilisha ibada ya Hijja kwenye mji mtakatifu wa Makka, Saudi Arabia, huku wito wa amani ukitolewa.
"Labeika Allahuma Labeika, Labeika la Sharika laka Labeika, Inna Lhamda Waniimata Laka Walmulku Laa sharika alaka." Waumini wa Kiislamu duniani wamejumuika kuitikia wito huo wa kumtukuza Mungu wao, wenye maana ya "Tunakuitikia Ewe Mola wetu tunakuitikia. Tumekuitikia ewe Mola usiye na Mshirika. Hakika wewe ndiye wa Kuhimidiwa. Neema zote ziko kwenye Utukufu wako. Hakika Wewe huna mshirika."
Ibada ya Hijja imekamilika na leo ni sikukuu, ambapo mahujaji wamerejea kutoka Mlima Arafat, ulio umbali wa kilomita 20 mashariki ya mji wa Makka na unaominiwa kuwa mtukufu kwa sababu, miongoni mwa mengine, ni mahala ambapo kiongozi wa Waislamu, Mtume Muhammad (S.A.W), alitoa hotuba yake ya mwisho.
Umati mkubwa wa mahujaji wa Kiislamu walipiga kambi usiku kucha katika jangwa kubwa linalouzunguka Mlima Arafat, lakini wengi wao walianza kuwasilli mwendo wa alfajiri. Wanaume, wanawake na watoto kutoka nchi 189 walifurika katika eneo hilo, wote wakiwa wamevalia mavazi meupe. Mahujaji wengine wameonekana wakiezeka mahema ambamo walilala usiku na kusali.
Baadhi ya waumini walijaribu kuupanda mlima huo, ijapokuwa hakuna visa vyovyote vya madhara vilivyoripotiwa.
Karibu Waislamu milioni tatu walisimama katika Mlima Arafat jana wakiomba msamaha kutoka kwa Mola wao. Hilo ni tukio la mwisho katika ibada ya Hija, ambayo ni nguzo ya tano ya Uislamu na ambayo ni wajibu kwa kila Muislamu mwenye uwezo kuutekeleza angalau mara moja katika uhai wake.
Ulinzi waimarishwa
Mahujaji katika mnara wa Minaa kwa ajili ya kitengo cha Jamarat, yaani kumrushia mawe Ibilisi. Mahujaji katika mnara wa Minaa kwa ajili ya kitengo cha Jamarat, yaani kumrushia mawe Ibilisi.
Maafisa wa Saudi Arabia wameimarisha ulinzi ukiwa na mamia ya vifaa vya upigaji picha na ukaguzi. Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani, Mansour al-Turki, alisema panatumika teklojia ya kisasa kuweza kuchukuwa hatua za haraka ikihitajika. Saudi Arabia ndicho kitovu cha Uislamu.
Katika khutba yake, Mufti Mkuu wa Saudi Arabia, Sheikh Abdul Aziz Al al-Sheikh, alisema viongozi wa Kiislamu wanawajibu wa kuwatumikia watu wao na kuhakikisha matatizo yanatatuliwa kwa kufuatana na mafundisho ya dini na sio matumizi ya nguvu na ghasia.
Kwa upande mwengine katika risala yake ya sikukuu ya Eid el Haj, kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Khamenei alionya kwamba umwagaji damu unaoendelea Syria unaweza kuzagaa katika nchi nyengine za Mashariki ya Kati.
Iran inaishutumu Uturuki na mataifa mengine ya Ghuba kwa kile inachokiita kuuchochea zaidi mgogoro wa Syria kwa kuwaunga mkono waasi wanaopigana na utawala wa Rais Bashar al-Assad, unaoungwa mkono na Iran.
Nchini Syria kwenyewe, makubaliano ya kusitishwa kwa mapigano kwa muda huu wa sikukuu kati ya waasi na serikali yanaripotiwa kuheshimiwa katika siku ya mwanzo ya Eid-el-Adh'ha.
Mahujaji kutoka Syria walionekana kwenye viwanja vya Mlima Arafat wakiwa na bendera kubwa ya waasi, kama ishara ya uasi ambao umedumu miezi 19 sasa nchini mwao, kupinga utawala wa Rais Assad.

0 Maoni:

Post a Comment