|
NGUVU ya vijana katika kutetea maslahi ya nchi na kuchochea maendeleo ni nyenzo muhimu sana katika taifa lolote lile kama vijana wenyewe watapewa nafasi ya kutumia vipaji vyao katika kuongoza jamii zao. Nguvu hiyo inajidhihirisha kwa wabunge vijana ambao wameingia bungeni na kuonyesha uwezo mkubwa wa kuongoza na kuleta mabadiliko wakifanya kazi bila woga. Wabunge kama Zitto Kabwe, January Makamba, Halima Mdee, Esther Bulaya na wengine wengi ni miongoni mwa vijana hao ambao wamekuwa wakileta changamoto bungeni bila kujali itikadi za vyama vyao. Katika makala haya Mbunge wa Viti Maalumu anayewakilisha kundi la Vijana Mkoa wa Mara, Esther Bulaya anasema kuwa alipoingia bungeni alikwenda na dhamira moja tu ya kushirikiana na vijana wenzake wa Mkoa wa Mara na taifa kwa ujumla ili kuleta maendeleo. “Nipo bungeni kuwawakilisha vijana na niko tayari kupoteza hata uhai wangu kwa kulitetea taifa langu hata kama nitaonekana msaliti katika chama changu kwa kukemea maovu,” anasema Esther na kuongeza: “Pamoja na kupoteza wazazi wangu nikiwa bado mdogo sikukata tamaa wala kupoteza matumaini ya kufanikiwa katika maisha yangu, na hiyo ni kutokana na maneno ya mwisho ya wazazi wangu ambayo yalinitia ujasiri wa kupambana na maisha ili kupata ushindi na kutimiza malengo yangu”. Anasema maneno ya mwisho ya wazazi wake kabla ya kufariki yalikuwa ni mbegu ya ujasiri wa kujituma, kutoogopa wala kukata tamaa katika kutafuta mafanikio hata katika hali ngumu ya upinzani na maadui wengi. Esther anasema akiwa darasa la sita, baba yake mzazi Amos Bulaya aliyekuwa askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wa cheo cha meja katika kambi ya Pangawe, Morogoro alifariki dunia na akiwa kidato cha pili, mama yake Hadija Ismail alifariki dunia pia. Baada ya wazazi wake kufariki dunia Esther alikuwa akilelewa na baba yake mdogo Paul Bulaya (Ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambaye alimsomesha hadi alipomaliza elimu yake ya sekondari na chuo. Akiwa Mbunge kijana wa CCM, Esther amekuwa amekuwa akishirikiana na wabunge wa vyama vya upinzani kiasi baadhi ya wabunge na viongozi wa chama chake wamekuwa wakimtuhumu kwa usaliti. Hata hivyo mwenyewe anasema anaamini kuwa kushirikiana na wabunge vijana ni kuimarisha nguvu ya kudai na kutetea haki za vijana. “Maendeleo hayaji kama hushirikiani na vijana katika uamuzi na utekelezaji, vijana wote bila kujali itikadi za vyama wanapaswa kuungana kukemea maovu na kupandikiza mbegu mpya ya ushindi na maendeleo ya nchi yetu,” anasema. Siasa Anasema akiwa shule ya sekondari Makongo aliteuliwa pia kuwa kiranja jambo ambalo liliwafurahisha hata ndugu zake hasa baba yake mdogo ambaye ndiye alikuwa akiishi naye kwa wakati huo. Mnamo mwaka 2000 alijiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari cha Morogoro, (MSJ) kuchukua Diploma ya uandishi wa habari ambako pia alikuwa Waziri wa Maendeleo ya jamii na Michezo. Jina la Esther lilianza kuonekana kwenye vyombo vya habari mwanzoni mwa miaka ya 2000 alipokuwa mwandishi katika kampuni ya Uhuru Publications Ltd inayochapisha magazeti ya Uhuru na Mzalendo. Esther aliyeingia bungeni baada ya kushinda nafasi za uwakilishi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Utekelezaji katika jumuiya hiyo anasema kazi kubwa anayofanya ni kushirikisha vijana katika kujiletea maendeleo yao. Anasema katika kipindi chote cha uandishi alikuwa akijifunza namna ya kujenga hoja na kuwasilisha na alipoona anaweza akajitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge. “Unajua kipindi chote nilikuwa najifunza kuwasilisha mawazo yangu ya kuijenga nchi kwa taaluma, na ilipofika mwaka 2010, niliona wazi kwamba hatua niliyofikia haitaweza kutimizwa kama sikuingia rasmi kwenye siasa na hasa kuwa mbunge.” Esther aliyeingia bungeni baada ya kushinda nafasi za uwakilishi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Utekelezaji UVCCM anasema kazi kubwa anayofanya ni kushirikisha vijana katika kujiletea maendeleo yao. Harakati za Ubunge kamili. Hata hivyo Esther amekuwa akitoa misaada mbalimbali katika mkoa wa Mara hasa katika michezo hali ambayo inatafsiriwa kama harakati za kuwania ubunge kamili katika jimbo la Bunda ambalo kwa sasa linakaliwa na Steven Wassira, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na uratibu). Esther aliingia bungeni baada ya kushinda nafasi za uwakilishi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), pia ni Mkuu wa Idara ya Utekelezaji UVCCM ambapo amejipanga kushirikisha vijana katika kujiletea maendeleo yao. Esther Bulaya alizaliwa miaka 32 iliyopita na ni mama wa mtoto mmoja (Briton, 7). Chanzo:Mwananchi | Na Dotto Kahindi
Wednesday, June 20, 2012
Bulaya: Niko tayari kufa nikitetea nchi yangu
Imeandikwa 11:20 AM na Steven Elias
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Maoni:
Post a Comment