Shirika la televisheni la Syria leo asubuhi limemuonesha rais wa nchi hiyo Bashar Al Assad, akihudhuria sala ya Idd ul Adha.
Hata hivyo licha ya utawala wa nchi hiyo kutangaza kusitisha mapigano,
katika siku nne ya kusherehekea siku hii kuu kwa waumini wa kiislamu,
bado kuna habari za kuendelea kwa mapigano .
Bashar Al Assad akionekana kuwa mtulivu na mwenye tabasamu kubwa
alihudhuria sala ya asubuhi ya Idd ul Adha katika msikiti mmoja mjini
Damascus. Hii leo pande zote mbili, serikali na makundi kadhaa ya waasi
yalikubaliana kusitisha mapigano kuanzia leo asubuhi hadi siku ya
jumatatu. Akitoa hotuba yake Imamu wa msikiti huo Walid Abdel Haq
alitaka wasyria kuwacha kuzozana kwa kuwa wote ni ndugu moja.
Imam Walid amesema mapigano na mauaji yameendelea kwa miaka miwili
nchini humo na ni lazima jambo hilo likomeshwe. Baada ya Sala hiyo Rais
Assad alionekana akisalimiana na waumini wengine huku akizungumza nao
kwa furaha.
Maandamano Syria
Maandamano ya kumpinga Rais Bashar Al Assad.
Hata hivyo licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano katika siku nne za
kusherehekea Idd ul Adha, maandamano ya kupinga utawala wa rais Bashar
yalifanyika. Hii ni kulingana na wanaharakati nchini humo pamoja na
mashirika ya kutetea haki za binaadamu. Maandamano hayo yametokea wakati
kukiwa kutulivu nchini Syria baada ya makubaliano ya kusitisha vurugu.
Kulingana na shirika la kutetea haki za binaadamu nchini Syria, kumekuwa
na mapambano kati ya vikosi vya serikali na waasi karibu na kambi moja
ya kijeshi kaskazini mwa mji wa Maaret al-Numan. Shirika hilo limesema
maandamano yametokea katika eneo moja la Raqa, kaskazini mashariki mwa
nchi hiyo ambapo vikosi vya serikali vimeripotiwa kurusha mabomu ya
kutoa machozi. Watu watatu wameripotiwa pia kujeruhiwa Katika eneo la
Daraa kusini mwa nchi hiyo baada ya polisi kufvyatua risasi hewani ili
kuwatawanya waandamanaji.
Nako mjini Idlib waandamanaji walisema kwa sauti, Ondoka rais Assad wewe
ni msaliti umeiharibu Syria. Hata hivyo upinzani ulitumia mtandao wa
kijamii facebook kuwataka watu nchini Syria waandamane, wakisema hatua
ya kusimamishwa mapigano ni nafasi kwao kuandamana kwa nguvu zote.
Mjumbe wa upatanishi Syria Lakhdar Brahimi
Kulingana na sheria za Syria ni kinyume cha sheria kufanya maandamano ya aina yoyote yale bila kupata kibali cha serikali.
Mpango wa kusimamisha mapigano ulizingatiwa baada ya mjumbe wa Umoja wa
Mataifa na hata jumuiya ya nchi za kiarabu kwa ajili ya Syria Lakhdar
Brahimi, kupendekeza hilo kwa pande zote mbili ili kutoa nafasi kwa
waislamu wa Syria kusherehekea iidi yao kwa amani. Tangu kuanza kwa
mapigano takriban miezi 20 iliopita watu zaidi ya 30,000 wameuwawa na
wengine wengi kupoteza makaazi yao.
0 Maoni:
Post a Comment