Friday, June 1, 2012

CCM watafunana


Ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkakati ulioshika kasi ni kama wasemavyo mitaani ‘ukimwaga mboga namwaga ugali’ kwani kila anayezungumza juu ya hali ya chama anajibiwa kwa pigo kubwa kuliko lake, kama inavyojidhihirisha baina kwa Mbunge wa Msalala, Ezekile Maige na Nape Nnauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho.

Siku moja tu baada ya Maige kumshutumu Nnauye kuwa ni gamba namba moja na kumtaka ajitafakari na kujiondoa kwenye nafasi hiyo kwa kuwa ameshindwa kusaidia chama kupata wanachama wapya na kuzuia wimbi la wanachama kutimkia upinzani, amejibiwa kwa kauli za kejeli na jeuri na Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Kahama, Marco Mipawa Ng’wanangolekwa, kuwa ana nongwa ya kuukosa uwaziri.

Jana Maige ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, lakini akatemwa na Rais Jakaya Kikwete pamoja na mawaziri wengne watano na naibu wawili katika uteuzi aliofanya Mei 4, mwaka huu, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa Nape aache tabia ya kutoa kauli ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaelekea kukidhohofisha chama.

Maige alitoa kauli hiyo juzi wakati akizindua matawi mawili ya wakereketwa wa CCM ambao ni wajasiriamali katika kijiji cha Isaka wilayani Kahama na kusema kuwa hivi sasa kuna wimbi kubwa la CCM kukimbiwa na wanachama.

Maige alimtaka Nape apime utendaji wake tangu alipoishika nafasi hiyo ni wanachama wangapi wamekwisha kujiunga na chama hicho, hivyo kuona kama anaimudu kazi yake.

Alisema mbali na Nape kushindwa kuzuia wimbi la wanachama kukihama chama hicho, pia alikwishatoa kauli ambayo haistahili kuvumiliwa na wana-CCM wenye uchungu na chama, ya kudai kuwa hata kama wanachama watahama wote yeye (Nape) hawezi kuhama na kwamba ni vema abaki peke yake na CCM haitakufa.

“Jamani Nape anachokifanya sasa ndani ya chama mimi ninaweza kuamini kwamba anatumika na kukidhi matakwa ya waliomtuma na siyo kwa manufaa ya chama,” alisema Maige.

“Kwa hali hii ambayo Nape amekifikisha chama hapa kilipo, ni vizuri sasa akajipima uwezo wake kama una tija gani ndani ya chama, ni vyema sasa akajiona mwenyewe kwamba yeye ni gamba namba moja na hivyo ni vyema akijivua badala ya kusubiri wana-CCM kumvua gamba lake,” alisema.

Ingawa juzi Nape hakutaka kujibizana na Maige kwa kudai kuwa yeye siyo saizi yake:
“Saizi yake ni kwenye wilaya, tawi na kata, huko ndiko watakakoshughulika naye.

Hivyo, sina muda wa kujibizana naye,” alisema Nape akikataa kuingia kwa undani juu ya madai ya Maige.

Hapana shaka ni kutokana na kauli ya Nape kauli ya Ng’wanangolekwa inatolewa ikisema wazi kuwa:

“Kama Katibu Mwenezi wa CCM wilayani Kahama kwa kutambua umuhimu wa vikao, na kwa kuheshimu mamlaka ya kikatiba ndani ya Chama, nimeona si vema kukaa kimya bila kutolea ufafanuzi tuhuma hizo ambazo kwa ujumla zinalenga kukivuruga na kukichafua Chama chetu.”

Katibu huyo anamkumbusha Maige kuwa CCM ina utaratibu wa kushughulikia masuala ya malalamiko mbalimbali ya wanachama na viongozi wake, lakini utaratibu alioutumia si wa CCM na kwamba haukubaliki kabisa kwani hauna nia ya kujenga isipokuwa kubomoa.

“Haya mapungufu anayoyasema leo Maige kayaona baada ya kunyang’anywa uwaziri? Nape na vikao vya kitaifa vya Chama chetu vinahusikaje na kufukuzwa kwake uwaziri na shutuma zinazomkabili za matumizi mabaya ya dhamana ya madaraka aliyopewa na rasilimali za nchi kama Waziri aliyekuwa na dhamana ya Maliasili na Utalii?” inahoji taarifa kwa vyombo vya habari ambayo hata hivyo ilisambazwa na Idara ya Itikadi na Uenezi inayoongozwa na Nape.

Katibu huyo amemkumbusa Maige kuwa busara inaonyesha kuwa kwa kuwa kikao kilichomtuhumu na kusababisha kuwajibishwa kwake ni Bunge, basi angepeleka malalamiko yake bungeni kwa ufumbuzi.

“Vinginevyo kama ana malalamiko yoyote juu ya utendaji wa vikao vya juu vya chama na Katibu Mwenezi wa CCM Taifa Ndg. Nape Nnauye angewasilisha kwenye Chama kwa kufuata utaratibu wa Chama chetu,” inasisitiza taarifa hiyo.

Katibu huyo ambaye hasemi kama taarifa hiyo ameitoa baada ya kukaa kikao na viongozi wenzake wa wilaya kwa kuwa CCM inaendeshwa kwa vikao kama anavyodai, amesema: “Tunakemea na kulaani utaratibu huu wa watu kukurupuka na kushutumu viongozi wa chama chetu kwa staili aliyotumia Maige.”

Ng’wanangolekwa anamtuhumu Maige kuwa lengo lake siyo jema na wala halina nia ya kujenga kwa CCM bali ni kubomoa.

“Nape anasemwa vibaya na watu wachache wasiowaadilifu kwa sababu ya uadilifu wake na kusimamia ukweli na msimamo wa vikao halali vya chama,” imesema taarifa hiyo.

Kurushiana makombora kwa viongozi, makada na wanachama wa kawaida wa CCM umekuwa ni mfumo mpya wa utendaji kiasi cha kuongeza mvutano wa makundi na uhasama ambao unakifanya chama hicho kupita katika kipindi kigumu.

Kikubwa kinachoelezwa kuwa nyuma ya mnyukano huu ambao hata Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, wiki hii amenukuliwa akisema kuwa makundi yanakiumiza chama hicho, ni mbio za urais mwaka 2015.

Juzi Maige ambaye amefuatana na Mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja, alihutubia maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Isaka na kuwaomba kumpa ushirikiano wa kutosha ili jimbo hilo lipate maendeleo endelevu na kuwaeleza waachane na siasa alizoziita kuwa ni za maji taka na za kupakana matope.

Mgeja naye aliwataka wananchi na wanachama wa CCM kumuunga mkono Maige kwa kuwa amefanya makubwa wilayani humo na kwa mkoa wa Sinyanga kwa ujumla.

Msimamo wa Mgeja unaonyesha dhahiri kuwa hawaivi na Katibu Itikadi na Uenezi wa Wilaya kimsimamo, hivyo kuonyesha picha nyingine ya mpasuko wa chama katika mkoa huo.

Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyowasilishwa katika mkutano wa saba wa Bunge na Mwenyekiti wake, James Lembeli, ikimtuhumu Maige kushindwa kudhibiti ubadhirifu katika wizara yake kama ulivyobainika katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii na usafirishaji wa wanyama hai nje ya nchi.

Mbali na Maige, mawaziri wengine walioachwa kutokana na tuhuma mbalimbali zilizotokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC); kwamba walishindwa kusimamia wizara zao na kuisababishia serikali hasara na wengine kutumia vibaya mabaraka yao.

Walioachwa ni Mustafa Mkulo (Fedha); Omar Nundu (Uchukuzi); William Ngeleja (Nishati na Madini); Dk. Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii) na Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara).

Manaibu mawaziri ni Athuman Mfutakamba (Uchukuzi) na Dk. Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii).

CHANZO: NIPASHE

0 Maoni:

Post a Comment