Katika kufatilia hali halisi ya mchakato wa kupata katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, nimeona nami nitoe maangalizo na maoni yangu binafsi.

Zanzibari imeshatunga katiba yake mpya. Je hii katiba ya muungano itagusa mabo yaliyomo katika katiba ya Zanzibari? Kama jibu ni ndiyo, basi hapa kuna kazi ya ziada, maana katiba ya Zanzibari inaweza kuimeza katiba mpya

Je kama wananchi watapenda zaidi mfumo wa serikali tatu. Nani atatengeneza rasimu ya serikali ya Tanganyika? Maana kuna uwezekano wa kuwa na mapendekezo ya serikali tatu kushamiri sana katika mchakato wa hii katiba mpya. Hii itasababisha haja ya kurasimu katiba mbili, yaana ya Tanganyika na ya Muungano.

Je kama wananchi watataka muungano upumzike, watakubaliwa au watafungwa kama wahaini. Kama watafungwa je huu mchakoto utakuwa huru kweli. Mimi napenda muungano uendelee, lakini labda wasioupenda ni wengi? Sijui? Je tume inajua?

Mwaka 1964 nilikuwa bado mdogo sana, lakini sikumbuki kama wananchi waliulizwa kuhusu, haja ya muungano, muundo, na mambo yake. Na kama kweli kuna mkataba wa Muungano, uko wapi? unasemaje? Je kuna tofauti kati ya mkataba wa muungano na hati ya muungano?

Inasemekana kuna hati zimefichwa, kama ni kweli ni kwanini? Muungano ni haki ya umma au serikali? Kama zipo, huu sio wakati muafaka wa kuzichapisha katika magazeti ya serikali? ili nasi tujue yaliyomo ili kuondoa haya mambo ya uvumi uvumi. Yanawapa watu visingizio vya kuzungumza mengiiii.

Naona kama kuna haja ya kuangalia vizuri sana huu mchakato wa katiba. Bado naamini kabisa ukifanyika vizuri utamjengea Raisi na bunge letu heshima kubwa sana kihistoria, na nchi kutupatia amani na maendeleo ya kudumu.

Nengeshauri, kwa hali ilivyo sasa, bila kutumia vitisho, maoni ya awali yakakusanywe Zanzibar (Pilot study), ili tume iweze kuwa na roadmap nzuri. Sikubaliani na vitendo vya kihuni, na nategemea vyombo vya sheria vinashughulikia. Ila nahisi kuna kitu cha kuangaliwa kwa umakini sana Zanzibar.

Nayasema haya kwa nia nzuri, nikiamini kutoka moyoni kwamba naipenda nchi yangu, na vizazi vyake vijavyo. Na ningependa sana amani ya kweli katika mfumo wa demokrasia ijengeke na kukomaa kadri miaka inavyoendelea. Bila katiba muafaka, nahisi matatizo makubwa mbele ya safari. Kuna haja sana ya kujikana nafsi zetu, katika suala la kutengeneza katiba mpya, yaani tunatikiwa kuwa wayakinifu zaidi, kuliko kubebwa na ushabiki wa aina yeyote ile.

Na:Fredrick Sanga