Saturday, May 19, 2012

Mpasuko watawala Kamati kuu Dodoma

KIKAO cha Kamati Kuu(CC) ya Chama Cha Mapinduzi jana kilitarajia kuendelea hadi majira ya usiku zikiwepo taarifa za mambo mazito kujadiliwa, huku suala la hali ya uchumi na mpasuko ndani ya chama likitawala kikao hicho.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenzezi, Nape Nnauye, jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa kikao hicho kingefanyika hadi usiku wa manane kutokana na kuchelewa kumalizika kwa Kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili.

“Ni kweli kwamba kikao cha Kamati Kuu kitafanyika hadi usiku sana hasa itakuwa kati ya saa sita au saba usiku maana kuna mambo makubwa na muhimu ambayo tunataka kuzungumza,’’alisena Nape.

Kwa mujibu wa Katibu huyo, miongoni mwa ajenda ambazo zilitarajia kupasua kichwa ndani ya kikao hicho ni pamoja na hali ya uchumi nchini Tanzania ambayo alisema itajadiliwa kwa mapana zaidi.

Alisema kuwa ajenda hiyo ni muhimu kutokana na ukweli kuwa mfumko wa bei kwa sasa unatisha na kuwafanya walala hoi kutokupata stahiki zao kikamilifu.

Hata hivyo, alibainisha kuwa mbali ya suala hilo, pia watajadili kwa mapana ajenda ya hali ya kisiasa ambayo alisema mara zote ni kudumu katika vikao vyao.

Kikao hicho kinafanyika huku, chama hicho kikiwa kimekumbwa na mpasuko mkubwa huku baadhi ya wanachama wake wakikihama na kuingia Chadema.

Tayari chama hicho kimepoteza baadhi ya viongozi wake akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho Mkoa wa Arusha, James Ole Millya na viomgozi wengine kutoka maeneo mbalimbaali ya nchi wamehamia chama hicho cha upinzani.

Nape alizitaja agenda zingine ambazo zitajadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na taarifa mbalimbali ndani ya chama, maendeleo ya uchaguzi ndani ya CCM pamoja na kuziba nafasi za makatibu wa mikoa wa chama hicho kutokana na uteuzi wa baadhi ya makatibu kuteuliwa na rais katika nafasi za ukuu wa wilaya.

Kwa upande mwingine Nape alikwepa maswali ya waandishi wa habari na kushindwa kueleza kwa mapana ajenda zingine na kusema kuwa hakuna mambo mengine makubwa zaidi yatakayojadiliwa zaidi ya aliyoyaeleza na kuwaeleza kuwa kesho wajumbe wa Halmashauri Kuu ndio watakaoamua zaidi.

Kwa muda wa siku tano sasa Sekretalieti ya chama hicho imekuwa na vikao vizito kwa ajili ya kuweka mambo sawa na leo kutakuwa na semina kwa kamati hiyo kabla ya kuanza kikao kesho.

chanzo;mwananchi

0 Maoni:

Post a Comment