Saturday, May 19, 2012

Shibuda: Nitatoboa siri za CHADEMA

MBUNGE wa Maswa Magharibu, John Shibuda (CHADEMA), ametishia kutoboa kile alichokiita siri za chama hicho kwa madai kuwa ameishazijua zote.

Aidha Shibuda amemtaka Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA), John Heche, amwombe radhi ndani ya siku tatu tangu leo (jana) kutokana na kauli za kumdhalilisha katika vyombo vya habari juu ya kutangaza nia yake ya kugombea urais 2015.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, mbunge huyo alidai kuwa iwapo Bavicha hawatamwomba radhi ndani ya siku tatu atatoa siri kubwa za vijana hao zilizofichika nyuma ya pazia.

“Niliingia CHADEMA ili kuelewa mfumo na kanuni za chama, sasa nimeisha zijua siri zao hivyo naweza kufanya jambo kwa wananchi wangu na Watanzania kwa ujumla. Lazima Heche anieleze ni kwa nini ametoa matamko katika vyomba vya habari ambayo yanalenga kunidhalilisha kwa wapiga kura wangu,” alisema.

“Sijui kama ni kauli ya vijana au yake mwenyewe na kama Heche ni kiongozi au mlinda masilahi ya viongozi ndani ya chama wenye fikra za ugandamizaji na ukabila ndani ya chama.”

Alisema kuwa mwenyekiti huyo anatakiwa kueleza anaendesha baraza hilo kwa mawazo ya wajumbe au anatumia cheo chake vibaya kwa lengo la kulida maslahi ya watu ambao ni wachache wenye fikra hasi.

“Kwani kuna nini mimi Msukuma wa watu nikigombea urais au hao Bavicha wana siri gani na wanamtaka nani awe Rais?” alisema na kudai anatangaza rasmi kwamba atagombea nafasi hiyo na kama atapitishwa na CHADEMA, atamteua Dk. Slaa kuwa meneja wake wa kampeni.

Mbunge huyo alidai kuwa hawezi kutoka CHADEMA, badala yake atapambana na kukabiliana na changamoto zote ndani ya chama hicho.

“Mimi sihami ndani ya chama lakini kama chama kitanikataa basi nitapeleka mashtaka yangu kwa wananchi ili niweze kuwaeleza kile kilichojificha nyuma ya pazia kwa Watanzania.

“Nilitoka CCM kwa lengo la kukataa kunyanyaswa; nikategemea kuwa huku hakuna mambo kama hayo, hivyo hata huku siwezi kukubali kuburuzwa kwa ajili ya maslahi ya watu wengine, na niliishamwambia Dk. Slaa kuwa siwezi kuburuzwa na kukubali dhuluma kwa ajili ya watu wachache badala ya kuwatetea Watanzania,” alisema.

Alidai kushangazwa na kauli ya Heche kutaka afukuzwe, akihoji itasaidia kuongeza matawi mangapi ya CHADEMA nchini, akidai alikataa kukubali fikra hasi hata alipokuwa CCM, hivyo hatakubali kufungwa mdomo kwa ajili ya watu wenye dhuluma, na wanaoendekeza ukabila na ukanda ndani ya chama.

Aidha alisema alipoulizwa ni kwa nini amekuwa akipingana na viongozi wenzake kwa mambo mengi, na hivyo kuzua migogoro, alisema hana mgogoro wowote ndani ya chama na kutaka kama ipo iwekwe wazi.

chanzo;Tanzania daima

0 Maoni:

Post a Comment