Friday, October 4, 2013

Warioba awa mbogo


  Amtaka kigogo wa CCM aseme kama ametumwa kuichafua tume
  Asisitiza amemsikia sana akiendesha kampeni ya kuchafua Tume
  1. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba
  2. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, amegeuka mbogo na kumtaka Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo, kuacha kupiga kelele dhidi yake kwa kuwa hakumtuma kazi ya kukusanya maoni ya katiba mpya, bali alitumwa na serikali kwa niaba ya wananchi.
    Jaji Warioba alitoa kauli hiyo jana kama karipio kwa Bulembo hilo jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, na kusisitiza kwamba Bulembo amekuwa na ajenda ya siri dhidi yake (Warioba) na baadhi ya wajumbe wa Tume kwa kuwa amekuwa akiwazungumzia wao binafsi kila anaposisimama katika majukwaa ya kisiasa.

    Alimtaka Bulembo kuthibitisha kuhusu kauli ambazo amekuwa akizitoa kwenye mikutano ya CCM katika mikoa ya Arusha, Tanga na Mbeya kuwa yeye (Warioba) amegeuka kuwa msemaji wa wananchi katika mchakato mzima wa kupata Katiba mpya.

    Jaji Warioba alitamtahadharisha Bulembo na kumtaka kuacha kupiga kelele pamoja na  kumshambulia badala yake azungumzie masuala yanayohusu Rasimu ya Katiba na siyo kuwajadili wajumbe.

    Aidha, Jaji Warioba alimtaka Bulembo kuthibitisha kama kauli ambazo alizitoa kwa nyakati tofauti katika mikoa hiyo ametumwa na CCM ama ni kauli zake binafsi.

    Jaji Warioba alisisitiza kuwa siku zote Tume yake imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na kuwataka wanasiasa akiwamo Bulembo kujadili Rasimu iliyotolewa badala ya Tume au wajumbe wake.

    Kwa mujibu wa Jaji Warioba, hakutumwa na CCM kufanya kazi anayoifanya na kwamba kazi hiyo alipewa na serikali kwa mujibu wa sheria na kwamba ataendelea kuifanya bila kusikiliza maneno yanayosemwa dhidi yake.

    Alikiri kuwa kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na Bulembo kwa nyakati mbalimbali zimechangia mchakato wa Katiba kuwa mgumu hususani wakati wananchi walipokuwa wakitoa maoni kupitia mabaraza ya katiba mkoani Mbeya.

    “Moja ya kazi za kisheria za Tume ni kutoa elimu kwa umma, na ni kazi ya wakati wote.  Sasa kama Bulembo anaona kutoa elimu ni dhambi ni sawa,” alisema Jaji Warioba  ambaye amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais.

    Kuhusu kukatishwa tamaa kutokana na kauli za wanasiasa hususani kutoka CCM ambao wamekuwa wakimuandama binafsi, Jaji Warioba alisema haogopi wala hatetereki kwa kuwa anafanya kazi aliyotumwa na wananchi.

    Alisema CCM iliishawasilisha maoni yake walipopewa nafasi ya kufanya hivyo, na kwamba masuala mengine yanayojitokeza zikiwamo kauli za Bulembo baada ya hapo hajui zinatoka wapi.

    Aliongeza kuwa Tume yake imekuwa ikifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kauli za wanasiasa mbalimbali na kuongeza kuwa pamoja na kauli hizo, inafarijika na kauli za kutia moyo wanazozipata kutoka kwa wananchi wa kawaida.

    “Nilisema mwishoni mwa mwezi uliopita, wanasiasa wamekuwa wakitoa matamshi yaliyoifanya kazi ya Tume kuwa ngumu katika mikutano ya mabaraza ya katiba,” alisema na kuongeza:

    “Matamshi mengine yalilenga Tume na wakati mwingine yalinilenga mimi binafsi au wajumbe wa Tume badala ya kuzungumzia rasimu,” alisema
    Warioba alisema siku zote Tume yake imekubali kukosolewa kwa kuamini kuwa kukosolewa ni jambo la kawaida, lakini alisisitiza kuwa ni vyema wananchi na wanasiasa wakajadili Rasimu ya Katiba iliyotolewa badala ya watu au Tume.

    “Nadhani wangezungumzia Rasimu wangetusaidia sana, badala ya kuzungumzia Tume na watu,” aliongeza.
    Juzi CCM iliendeleza kauli zake zinazoonyesha kumuingilia na kumshambulia vikali Jaji Warioba na kumtaka aache kuwasemea Watanzania juu ya aina ya Katiba wanayoitaka.

    Matamshi ya kumshambulia Jaji Warioba yalitolewa mkoani Tanga na Bulembo, wakati akihutubia moja ya mikutano ya hadhara ya wanachama wa chama hicho.

    Bulembo alinukuliwa katika vyombo vya habari akisema kuwa siyo sahihi kwa Jaji Warioba kuwa msemaji wa Watanzania kuhusiana na mambo wanayoyataka yaingizwe ndani ya katiba.

    “Jaji Warioba ni mmoja kati ya Watanzania mamilioni na kwa hali hiyo hawezi kubeba mawazo ya Watanzania wengine, ni vizuri akasimamia Rasimu, badala ya kuwa msemaji wa wananchi,” alisema Bulembo ambaye pia ni Mjumbe wa kamati Kuu (CC) ya CCM.

    Kauli hiyo ya Bulembo imetolewa wakati kukiwa na msuguano kati ya CCM na serikali yake kwa upande mmoja, na vyama vitatu vya upinzani vyenye wabunge ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

    Mwishoni mwa mwezi uliopita, Jaji Warioba akizungumza na waandishi wa habari, aliwakemea baadhi ya viongozi wa kisiasa kwa kuiingilia mchakato wa kupata Katiba mpya unaoendelea.

    Alisema baadhi ya changamoto zilizojitokeza wakati wa kuendesha Mabaraza ya Katiba, ni kwa baadhi ya vyama vya siasa kuingilia uhuru wa wajumbe katika kutoa maoni kuhusu Rasimu ya Katiba, wakiwafundisha nini cha kusema.

    Jaji Warioba aliwasihi viongozi wa vyama vya siasa kuwaachia wananchi, cha kusema kwani, katiba inayotafutwa ni ya wananchi, na si ya vyama au kundi fulani

    Bulembo alipotafutwa jana kufafanua kama kauli hizo ni zake binafsi au ametumwa na CCM,hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila majibu.
  3. Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms),pia hakujibu hadi tunakwenda mitamboni
     
CHANZO: NIPASHE

0 Maoni:

Post a Comment