Sunday, January 20, 2013

Nape atakiwa kufuta kauli yake

na Betty Kangonga BAADHI ya viongozi wa dini nchini 
wamemtaka Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kufuta kauli yake ya kuhusisha kanisa na masuala ya ufisadi yanayotokea nchini. Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Haki za Binadamu kwa Jamii, Mchungaji William Mwamalanga, alisema kuwa kauli iliyotolewa na kiongozi huyo dhidi ya kanisa ni ya uchonganishi kwa jamii. Mwamalanga alisema kuwa kutokana na kauli hiyo wamemtaka kiongozi huyo kuliomba radhi kanisa ndani ya saa 48 kwa kitendo hicho cha kulihusisha kanisa la ufisadi. “Hawezi kusema kuwa kanisa la hapa nchini ndilo linachangia Watanzania kukosa dawa katika hospitali zetu kwa madai kuwa tumekuwa tukipokea watu wanaohusishwa na ufisadi,” alisema. Alisema kuwa iwapo Nape atagoma kufuta kauli hiyo basi suala hilo watamuachia Mungu kwa kuwa kisasi ni juu yake. Mwamalanga alisema kuwa shutuma alizotoa kiongozi huyo zingekuwa na maana iwapo angekuwa nje ya chama hicho ambacho kimekuwa mstari wa mbele kupigania suala hilo lakini limeshindwa kufanikiwa. “Huyu tunajua alikuwa akimlenga nani katika kipindi hicho cha Meza ya Busara kilichorushwa na redio moja ya jijini, kama Nape anamuona kiongozi huyo ni fisadi basi atoke ndani ya chama hicho lakini si kuendelea kuweka uchonganishi dhidi ya kanisa,” alisema. Mwamalanga ambaye anaongoza kamati hiyo ambayo ina viongozi wa madhehebu zaidi ya 215, alisema kuwa kanisa halitambagua mtu kwa kuwa limekuwa ni kimbilio la watu wote.

0 Maoni:

Post a Comment