Afisa mmoja mashuhuri wa kijasusi nchini Lebanon anayeupinga utawala wa
Rais Bashar al - Assad, jana aliuawa katika mripuko mkubwa wa bomu la
kutegwa ndani ya gari katika mji mkuu Beirut
Tukio hilo ni dalili nyingine inayoonyesha kuwa vita vya wenyewe kwa
wenyewe nchini Syria vinaiingiza nchi hiyo jirani, Lebanon, katika
mgogoro huo. Wissan al-Hassan, ambaye aliongoza uchunguzi uliozihusisha
Syria na kundi la Hezbollah katika mauwaji ya Waziri Mkuu wa zamani
Rafik al-Hariri, na watu wengine saba waliuawa jana wakati bomu
liliporipuka katikati ya mji wa Beirut.
Upinzani wailaumu Syria
Mlipuko ulitokea katika wilaya ya Ashafriyeh, katikati mwa Beirut
Viongozi wawili wakuu wa Upinzani wamemlaumu Rais wa Syria Bashar
al-Assad kwa shambulizi hilo, ambalo limeshutumiwa vikali na jamii ya
kimataifa. Na Makundi amwili makuu ya upinzani nchini humo, baada ya
mkutano wa dharura jana, yakaitaka serikali ya Lebanon kujiuzulu. Katibu
Mkuu wa kundi la Future Movement Ahmad Hariri alisema serikali ni
sharti ijiuzulu na Waziri Mkuu Najob Mikati ni lazima aondoke.
Marehemu Hassan alikuwa na uhusiano wa karibu na mwanawe Hariri, Saad,
ambaye ni kiongozi wa upinzani na anayepinga utawala wa Assad. Waziri wa
Habari wa Syria Omran al-Zohbi alilaani kile alichokitaja kuwa ni
“shambulizi la kigaidi” akisema matukio kaam hayo hayakubaliki kamwe.
Saad Hariri na Walid Jumblatt, kiongozi wa chama cha Druze cha Lebanon,
waliishutumu serikali ya rais wa Syria kufanya shambulizi hilo.
Shutuma za jamii ya kimataifa
Lakhdar Brahimi anatafuta uungaji mkono kuhusu pendekezo lake la kusitisha mapigano Syria
Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Marekani, Uingereza na Ufaransa
wote wameshutumu shambulizi hilo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki
Moon alivitaka vyama vyote vya Lebanon kutochochewa na tukio hili la
kinyama. Nayo taarifa ya Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya
Catherine Ashton ilisema waliohusika na uhalifu huo ni lazima wasakwe na
kufunguliwa mashitaka.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton alilaani vikali
shambilizi hilo, akisema kuawawa mkuu wa kijasusi wa jeshi la ndani la
Lebanon, Jenerali Wissam al-Hassan ni dalili mbaya kuwa kuwa wale ambao
wanaendelea kuhujumu utulivu wa Lebanon.
Brahimi yuko Damascus
Wakati huo huo, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kiarabu kuhusu
mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi amewasili mjini Damascus jana ambapo
anatarajiwa kufanya mazungumzo ya kuweka chini silaha wakati wa siku kuu
ya Waislamu, baadaye mwezi huu. Msemaji wa Brahimi, Ahmed Fawzi alisema
mjumbe huyo wa amani atakutana na rais wa Syria Bashar al-Assad hivi
karibuni. Vyombo vya habari vya serikali viliripoti kuwa Brahimi
atakutana na Waziri wa Mambo ya Kigeni Walid al-Muallem hii leo.
Brahimi, anapendekeza mapigano yasitishwe kati ya serikali ya Syria na
waasi wakati wa sherehe za siku kuu ya Kiislamu, Eid al-Adha, ambayo
inaanza Oktoba 26. Serikali ya Syria na upinzani zimeelezea nia yao ya
kuwa tayari kusitisha mapigano. Brahimi amewasili Syria baada ya kuzuru
Saudi Arabia, Uturuki, Iraq, Misri, Lebanon na Jordan kutafuta uungaji
mkono wa pendekezo lake. Pia alizuru Iran, mshirika mkuu wa utawala wa
Assad.
0 Maoni:
Post a Comment