Mhe:John Mnyika
MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) ameahidi kufuatilia utungwaji wa sheria ya udhibiti wa kodi za pango itakayounda mamlaka ya udhibiti wa kodi za nyumba na gharama za vifaa vya ujenzi.

Mnyika ametoa ahadi hiyo jana katika taarifa aliyoituma kwa vyombo mbalimbali vya habari ikieleza kuwa ahadi hiyo inatokana na maombi ya taarifa ya Chama cha Wapangaji wa Shirika la Nyumba (CHAWASHINYU) katika mkutano wa wapangaji wa Shirika la Nyumba uliofanyika Jumapili ijayo jijini Dar es Salaam.

Mnyika alisema ibara ya 63 ya Katiba imeweka wazi kuwa wabunge wanapaswa kuisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi na kutunga sheria hivyo ameitikia mwaliko wa mkutano huo kutimiza wajibu huo na kuchukua kazi hizo kibunge kwa kuwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi haijawasilisha bungeni sera na sheria kama ilivyoahidi.

“Awali wakati uchumi wa nchi unaendeshwa na dola kulikuwa na udhibiti wa kisheria. Hata hivyo, baadaye sheria hizo zikafutwa kwa kisingizio cha nchi kufuata mfumo wa soko huru lakini ukweli ni kuwa hili la sasa sio soko huru, ni soko holela kwa kuwa hata soko huria lina sheria na kanuni ikiwemo udhibiti,” alisisitiza Mnyika.

Mnyika alisema ongezeko kubwa la kodi za nyumba na gharama za vifaa vya ujenzi ni matokeo ya udhaifu wa kisera, kimfumo na kitaasisi katika sekta ya nyumba na makazi.

Aidha alisema katika mazingira ya sasa ya upungufu wa nyumba hususani mijini na gharama za juu za ujenzi, bila kuwa na mfumo wa udhibiti, mzigo mkubwa utawaelemea wananchi sio wapangaji wa Shirika la Nyumba (NHC) pekee, bali wakazi wengi.

Alisema suala hilo limeshajadiliwa bungeni ambapo awali mwaka 2011 liliwasilishwa bungeni na Waziri Kivuli wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Halima Mdee ambapo Kambi ya upinzani iliitaka serikali iweke utaratibu utakaotambulika kisheria utakaoweka mwongozo.

Hata hivyo, aliyekuwa wa kwanza kuwasilisha hoja binafsi ya suala hilo, alikuwa Mbunge wa Bumbuli, January Makamba (CCM), kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia.

Mnyika alisema atamtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi atoe kauli hatua iliyofikiwa katika mchakato wa kukamilisha sera ya nyumba na kuandaa muswada wa sheria husika na lini azimio hilo la bunge litatekelezwa kwa ukamilifu.