Na Egbert Mkoko, Grahamstown, Afrika Kusini
NAOMBA nianze makala haya kwa kuelezea kisa kilichotokea hapa Afrika Kusini mwaka 2006 kikiihusisha shirika la utangazaji nchini humu SABC, na kutawala vyombo vya habari kwa muda wa karibu nusu mwaka, kuanzia Juni mwaka huo hadi mwezi wa Desemba.
SABC iliingia katika msukosuko mkali baada ya gazeti moja maarufu liitwalo Sowetan kuvujisha habari za Mkuu wa Kitengo cha Habari ndani ya SABC, Dk. Snuki Zikalala, kuwapiga marufuku wanaharakati kadhaa kushiriki katika vipindi mbalimbali vya redio na televisheni.

Habari hiyo iliandikwa katika gazeti la Sowetan Juni 20 mwaka 2006, na iliwashtua raia wengi wa Afrika Kusini, kutokana na demokrasia iliyoanza kuota mizizi nchini humu, na hasa pale chombo cha habari cha umma kinapochukua hatua ya aina hiyo.
Kabla sijaendelea na kisa hiki, naomba tuwekane sawa kwamba SABC si chombo cha habari cha Serikali (state or government owned broadcasting) hapa Afrika Kusini, bali ni chombo cha habari cha umma (public broadcasting service) ambacho kimeanzishwa kwa mujibu wa sheria ya utangazaji namba Nne ya mwaka 1999.

Kutokana na hali hiyo, chombo hiki si mdomo wa Serikali na hilo limewekwa bayana katika sheria ya utangazaji na sera ya SABC.
Tuendelee na kisa chetu. Ni kwamba Dk. Zikalala kwa siri kuanzia mwaka 2005, alikuwa akiwapiga marufuku wanaharakati mmoja baada ya mwingine kuhudhuria vipindi vya mahojiano na majadiliano ambavyo vilikuwa vikiandaliwa na SABC.

Kila mmoja alikuwa akipigwa marufuku kutokana na sababu tofauti. Wapo waliopigwa marufuku kwa madai ya kuukosoa utawala wa Rais wa wakati huo Thabo Mbeki, utawala ambao ulikuwa katika msukosuko mkubwa kuanzia ndani ya chama tawala ANC hadi nje kwa maana ya serikalini.

Pia wapo waliopigwa marufuku kwa madai ya kuukosoa utawala wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, mambo ambayo Dr Zikalala aliyewahi kuwa kada wa ANC huko nyuma hakukubaliana nayo.

Wanahabari katika shirika hilo la utangazaji wengi wao hawakuifurahia hatua ya bosi wao huyo kuwafungia wanaharakati, hatua ambayo ilikuwa ni kinyume cha sera ya shirika.

Kuvuja kwa habari hiyo, kulimfanya Afisa Mtendaji Mkuu wa SABC wakati huo, Dali Mpofu kuunda tume ya uchunguzi kuthibitisha madai hayo yaliyoibuliwa na Sowetan.

Sitakwenda ndani zaidi kuelezea nini ambacho tume ilikibaini ndani ya uchunguzi wake huo ambao ulikamilika ndani ya wiki nne tu.
Lakini si mbaya pia nikikupa mkasa mwingine uliotokea ndani ya SABC ikiwa ni sehemu pia ya kisa hicho.

Baada ya Sowetan kuandika habari hiyo na kabla ya tume kuundwa, msemaji wa SABC, Kaizer Kganyago alitoa taarifa ya kukanusha kuwapo kwa mwanaharakati yoyote aliyepigwa marufuku kushiriki vipindi kwenye shirika hilo na taarifa hiyo aliitoa siku moja baadaye yaani Juni 21, 2006 wakati akihojiwa na mtangazaji wa redio iliyo chini ya SABC iitwayo SA FM.

Wakati Kganyago akikanusha, mtangazaji wa kipindi John Perlman, akamwambia moja kwa moja msemaji huyo kuwa kwanini anakanusha kitu ambacho ni kweli kimetokea na kinaendelea kutokea, na yeye (mtangazaji) amewahi kushuhudia mgeni wake akitolewa studio kwa madai kama yalivyoandikwa na Sowetan!

Hali ya hewa studio ikachafuka na utata ukaongezeka juu ya ukweli wa hatua ya SABC kufungia wanaharakati, huku mtangazaji huyo akiwa na ushujaa wa ajabu kuendelea kumuumbua hewani bosi wake dhidi ya ‘uongo’ anaoutetea.

Hatimaye ukweli uliwekwa bayana kuwa uamuzi wa aina hiyo ni kweli yalichukuliwa na ni kinyume cha sera na kanuni za SABC kama shirika la utangazaji la umma.

Licha ya ripoti kufichwa kwa miezi kadhaa hadi hadi baada ya kelele za wadau mwishoni mwa mwaka huo wa 2006, lakini funzo kubwa lilipatikana kutokana na uozo huo uliokuwapo ndani ya SABC.

Nimechukua kisa hiki cha Shirika la Utangazaji Afrika Kusini makusudi ili kuangalia ni wapi shirika letu la utangazaji Tanzania (TBC) lilipo na ni wapi linatakiwa kuelekea.

Kwa sasa, ni dhahiri kwamba TBC si shirika la umma, ni shirika linalomilikiwa na Serikali. Nina uwezo wa kulithibitisha hilo!
Kwa mujibu wa sura ya pili kifungu cha nne, kifungu kidogo cha pili katika Sera ya Habari na Utangazaji Tanzania ya mwaka 2003, Serikali inajipa haki ya kuendelea kumiliki na kuimarisha vyombo vyake vya habari (kwa maana ya redio, televisheni na magazeti) huku kifungu cha saba katika sura hiyo ya pili kikieleza malalamiko ya Serikali kutokana na televisheni na redio binafsi kushindwa kujiunga na vituo vya ‘serikali’ katika kurusha matukio muhimu ya kitaifa.

Sera hii ya habari na utangazaji ambayo ndiyo inatumika hadi sasa, ni ushahidi tosha kuwa walau kwa sasa, Serikali haina mpango wa kuhakikisha kunakuwapo na chombo cha habari ambacho ni mali ya umma. Hivi vilivyopo sasa ni mali halali ya Serikali.
Kuna tofauti kubwa sana ya chombo cha habari cha Serikali na kile cha umma. Kwa kutumia mfano ule wa SABC, chombo cha habari cha Serikali kinapaswa kufanya kazi kwa maslahi ya Serikali na si vinginevyo.

Hakilazimiki kufuata maslahi ya umma, na hii inamaanisha kwamba, kama nchi itakuwa chini ya utawala wa kiimla, basi mwananchi wa kawaida hana pa kukimbilia kutika kuikosoa Serikali iliyo madarakani.

Gazeti la Sowetan liliamua kuandika habari ile kwa sababu lilitambua fika kuwa SABC ilikuwa imefanya uamuzi kinyume cha wajibu wa chombo cha habari cha umma.

Katika Televisheni au redio ya umma, hakuna mwenye haki ya kumzuia raia kutoa hisia zake ili mradi taratibu za kawaida ndani ya redio au TV husika zimefuatwa. Ilichofanya SABC kupitia kwa Dk. Zikalala ilikuwa ni kinyume cha kanuni na ndiyo sababu aliadhibiwa kwa kosa hilo.

Chombo cha habari cha Serikali ni mdomo wa Serikali. Kila linalotoka serikalini hata kama halina maslahi kwa umma ni lazima lipewe nafasi katika chombo hicho.

Ni juu yako mwananchi ukitaka sikiliza/angalia ukitaka acha lakini lazima litangazwe maana Serikali ndiye mmiliki wa chombo hicho. Kwenye chombo cha habari cha umma, hilo halina nafasi kwani ni ‘umma kwanza’ na wala si ‘serikali kwanza’.

Chombo cha habari cha umma hakitakiwi kuwajibika serikalini, TBC yetu inawajibika moja kwa moja serikalini chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Ni lazima kutafuta namna ya uwajibikaji ikiwa kuna nia ya kuanzisha chombo chetu cha umma.
Mfano SABC inawajibika moja kwa moja bungeni na hata afisa mtendaji wake mkuu hateuliwi na Rais kama ilivyo kwa TBC yetu.
Wakati wa utawala wa Tido Mhando ndani ya TBC, kulikuwapo na dalili za mbali kutaka kuibadilisha TBC walau kuelekea kuwa kama chombo cha umma licha ya kwanza vikwanzo vilikuwa bado vimejaa barabarani na safari ilikuwa ni ndefu sana.
Sasa TBC ina utawala mpya chini ya Clement Mshana.

Pengine nimpongeze Mshana kwa kuteuliwa kwake. Lakini mwisho kabisa naomba kutoa hoja kwamba; Mshana, Tanzania haina shirika la utangazaji la umma, Watanzania hawana sehemu ya kwenda kutoa hisia zao, Watanzania hawana chombo kinachofanya kazi kwa matakwa yao, kwa maslahi yao na chini ya umiliki wao kama umma, na ukweli ni kwamba sasa ni wakati muafaka kwa watanzania kuwa na shirika au chombo chao cha utangazaji.

Naamini huu ni wakati mwafaka chini ya utawala wako, kuhakikisha TBC inabadilika kutoka kuwa chombo cha habari cha Serikali, kutoka kuwa mdomo wa Serikali, kutoka kuwa kipaza sauti cha Serikali, na badala yake kuwa chombo cha habari cha umma kwa maslahi ya Watanzania wote. Naomba kutoa hoja! By Egbert Mkoko.