VIGOGO 10 wametajwa kuhusika katika kashfa ya kuficha Sh303.7 bilioni katika benki mbalimbali nchini Uswisi.
Katika orodha hiyo inadaiwa kuwa yupo kiongozi mmoja mwandamizi mstaafu,
maofisa watatu wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
mawaziri wastaafu ambao baadhi yao bado ni wabunge na aliyewahi kuwa
kiongozi mwandamizi wa Benki Kuu Tanzania (BoT).
Majina hayo ambayo mwandishi wetu amefanikiwa kuyaona, yamo katika
orodha ya mchunguzi mmoja wa kimataifa wa masuala ya ufisadi (jina
tunalo).
Juzi, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alimshukia Mkurugenzi Mkuu
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward
Hoseah akimtuhumu kuandika barua Uswisi akisema Tanzania haina masilahi
na mabilioni ya fedha yaliyofichwa katika benki zilizopo nchini humo.
Hata hivyo, Dk Hoseah alikanusha madai hayo akisema hajawahi kufanya
hivyo.
Akizungumza jana Zitto alisisitiza kauli yake akisema: “Sijawahi kumsema
Dk Hoseah kwa lolote, kwa nini leo nimsingizie? Yeye mwenyewe anajua
ushirikiano niliompa wakati wabunge wanapinga yeye asichunguze malipo ya
posho mara mbili kwa wabunge.”
“Nilisimama kidete kusema Takukuru wapo sahihi na mimi nilikwenda
mwenyewe kwao kuhojiwa na kuagiza wajumbe wa kamati yangu (Kamati ya
Bunge ya Mashirika ya Umma), waende kuhojiwa. Spika aliyestaafu (Samuel
Sitta) akaizima kashfa ya wabunge kupokea posho mara mbilimbili.
Mwulizeni amesahau? Sasa leo nimzushie ili iwe nini?.”
Alisema orodha ya Watanzania wenye fedha huko Uswisi, ipo na ameiona na nyaraka zinaweza kutolewa kwa taasisi za Serikali tu.
“Dk Hoseah kazuia nyaraka hizo. Akitaka nimwonyeshe mtu anayeweza kutoa
nyaraka hizo, nipo tayari isipokuwa aahidi kuiweka wazi,” alisema
Zitto.
Alisema katika orodha ambayo Waziri wa Fedha wa Ufaransa anayo, kuna
Watanzania lakini akaituhumu Serikali akisema haitaki kufuata njia
halali za kupata orodha hiyo kwa kuwa viongozi wengi na wafanyabiashara
wakubwa wana akaunti katika benki za Uswisi.
Juni 26, mwaka huu gazeti hili lilichapisha habari kuhusu utoroshwaji wa
fedha hizo na kueleza kuwa Polisi wa Kimataifa (Interpol) nchini kwa
kushirikiana na Takukuru inachunguza suala hilo.
Kiasi hicho cha fedha kimedaiwa kuingizwa katika akaunti za Watanzania
na kampuni moja ya uchimbaji mafuta na kampuni kadhaa za uchimbaji
madini ambazo zinafanya kazi Tanzania.
Chanzo hicho kiliongeza kwamba kiasi hicho cha fedha kipo katika akaunti
sita tofauti zinazomilikiwa na Watanzania wakiwamo wanasiasa wakubwa.
Hata hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa tangu akaunti hizo zifunguliwe, wamiliki wake halali hawajawahi kuingiza hata shilingi.
“Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa fedha hizo zipo katika akaunti sita
tofauti ambazo zinamilikiwa na wanasiasa wakubwa nchini na wenzetu wa
Uswisi wameeleza fedha hizo zimeingizwa na kampuni kadhaa ambazo
zinahusika na mafuta pamoja na madini hapa nchini,” kilidokeza chanzo
hicho.
Kugundulika kwa kiasi hicho cha fedha katika benki za Uswisi ni kutokana
na ripoti ya Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB) iliyotolewa mwaka huu.
0 Maoni:
Post a Comment