
Chama tawala cha Ukraine leo kimedai kushinda katika uchaguzi wa bunge
uliofanyika jana, huku matokeo ya awali yakionyesha kinakabiliwa na
ushindani kutoka kwa vyama pinzani vya Vitaly Klitschko na Yulia
Tymoshenko.
Waziri Mkuu wa Ukraine Mykola Azarov ameelezea uhakika wake kwamba chama
tawala kitashinda viti vingi katika bunge jipya baada ya uchaguzi wa
jana, ambao mataifa ya Magahribi yanaona ni mtihani mkubwa kwa
demokrasia ya Ukraine kutokana na kufungwa kwa mpinzani wa Rais Victor
Yanukovich.
Chama cha Rais Yanukovich kimepata asilimia 35.6 ya kura dhidi ya asilimia 21.5 ilizopata chama cha upinzani cha Tymoshenko. Katika taarifa yake, tume ya uchaguzi imezingatia asilimia 40 ya kura zilizopigwa kwa mfumo sawa wa kuamua viti nusu vya bunge jipya. Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa chama hicho tawala pia kilitarajiwa kushinda angalau viti 110 kati ya 225 vya bunge. Akielezea kuhusu uchaguzi huo Azarov amesema wanategemea kuwa chama tawala kitapata viti vingi katika bunge jipya. Aidha, chama cha kikomunisti kilikuwa kimeshika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 15.1ya kura na chama kipya cha UDAR kilichojitenga na Klitschko kikiwa kimepata asilimia 12.8.
Urusi na Umoja wa Ulaya wanaufatilia uchaguzi huo
Uchaguzi huo wa jana ni mkubwa wa kwanza kufanyika nchini Ukraine ambao umeonyesha mvutano kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi tangu kiongozi aliyefanya mapinduzi ya chungwa mwaka 2004, Tymoshenko kushindwa katika uchaguzi wa urais mwanzoni mwa mwaka 2010, uchaguzi uliomuweka madarakani Yanukovich. Urusi inaufatilia uchaguzi huo kwa makini, huku Umoja wa Ulaya ukitaka viwango vya demokrasia vizingatiwe, wakati ambao Ukraine inaendelea kusisitiza nia yake ya kujiunga na umoja huo. Waangalizi wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya-OSCE wanatarajia kutoa maamuzi yao kuhusu uchaguzi huo baadae hii leo, ambayo yanafatiliwa kwa karibu kabisa kuona iwapo kuna udanganyifu uliofanywa.

0 Maoni:
Post a Comment