Wednesday, June 6, 2012

Msimamo wa Mheshimiwa Wenje juu ya Mwenyekiti wa NCCR.


Wenje achachamaa
MBUNGE wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (CHADEMA), amesema kamwe hatakiomba radhi Chama cha NCCR-Mageuzi kwa kuwa anaamini Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa mbunge na Rais Jakaya Kikwete hana ujasiri wa kuikosoa serikali.

Wenje alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na Tanzania Daima kuhusu tamko la Chama cha NCCR-Mageuzi kumpa mwezi mmoja kuwaomba radhi kutokana na kauli dhidi ya Mbatia kwamba chama hicho ni CCM B.

Alisema hata wakimpa mwaka mzima, hataomba radhi kwa kuwa anaamini katika msimamo wake.
“Naomba nitoe msimamo wangu kwamba mimi Wenje nilitoa maoni kama Wenje na si kwa niaba ya CHADEMA na kama Mtanzania mwenye haki ya kutoa maoni yake.

“Kauli niliyosema na narudia na sijutii na sifuti ni kwamba Mbatia ambaye ni mpinzani, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi kuteuliwa na Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM kuwa mbunge, maana yake Kikwete amempa ajira ya kwenda bungeni,” alisema.

Wenje alidai kuwa Mbatia hawezi kuwa jasiri wa kusimamia na kukosoa serikali ya Kikwete ndani ya Bunge, ambaye ndiye amempa mamlaka na ajira ya kuja bungeni.

“Yani hapa duniani, hakuna mtu aliyewahi kuwa mkali dhidi ya bosi wake. Huu ujasiri utautoa wapi? Mimi bosi wangu ni watu wa Nyamagana walionipigia kura na CHADEMA walionipa ridhaa ya kugombea. Leo hii mimi siwezi kusimama ndani ya Bunge nikaipiga CHADEMA mkwara.

“Hivyo hivyo wabunge wa Viti Maalumu wanafanya kazi kwa niaba ya vyama vyao. Kwa hiyo Mbatia mamlaka yake ya kuja bungeni yametokana na huruma, fadhila na utashi binafsi wa Rais Kikwete, sasa haiwezekani Mbatia kuwa na ujasiri wa kuikosoa serikali yake. Hapa ni kudanganyana na mimi kama Wenje msimamo wangu ndio huo,” alisema.

Aidha, alikanusha madai kuwa amekiita chama hicho CCM B na kusisitiza kuwa alichosema ni kutokuwa na imani na Mbatia.

Chama hicho, kimesema kuwa ndani ya mwezi mmoja endapo Wenje hataomba radhi kitamburuza mahakamani.


by Gwalihenzi;

0 Maoni:

Post a Comment