Sunday, June 3, 2012

Maige aitabiria Chadema ushindi 2015

Mnyika ataka Mkuchika aadhibiwe

Ezekiel Maige

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, amesema mabadiliko ya mawaziri yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete, yamepanua wigo mkubwa kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupata ushindi.

Maige amesema Chadema kinachozidi kupata nguvu na kuungwa mkono, kinaweza kulichukua jimbo la Msalala ambalo yeye ni Mbunge wake, kutokana na hatua iliyofikiwa, kumuweka kwenye orodha ya watuhumiwa wa ufisadi.

Wakati Maige akisema hayo, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika amewataka wapiga kura wa Newala mkoani Mtwara, kumwadhibu Mbunge wa jimbo hilo, George Mkuchika kwa kushindwa kudhibiti vitendo vya kifisadi kwenye halmashauri za nchini, ikiwemo Newala.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kutoka jimboni Msalala, Maige alisema kitendo cha kutuhumiwa, kisha Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuridhia Rais Kikwete kufanya mabadiliko ya mawaziri, hakikustahili.

“Unajua kitendo cha kuhukumiwa na Kamati Kuu (CC) ya chama kwamba nifukuzwe Uwaziri, hata bila kunisikiliza, hakikuwa cha kistaarabu,” alisema Maige.

Maige alitoa mfano kuwa aliyewahi kuwa Mbunge wa Ludewa na Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba, aliwahi kushutumiwa lakini akapewa nafasi ya kujitetea, hivyo kuadhibiwa kwake kulifanyika pasipo kupewa nafasi ya kujitetea.

Alifafanua kuwa ikiwa CCM itampitisha tena kuwania ubunge wa jimbo hilo, upinzani hususani Chadema watapa mwanya wa kumshambulia kwamba yeye (Maige) ni fisadi, huku wakijenga msingi wa hoja yao kwenye hatua ya kufukuzwa kazi na Rais Kikwete.

Pia alisema ikiwa jina lake halitarejeshwa, wapinzani watapa mwanya wa kuisema CCM kwamba ni chama cha mafisadi, na kuwa hata akiletwa mgombea mwingine atachukuliwa kuwa anatoka kwenye kundi la mafisadi wale wale.

“Kwa hiyo utaona kwamba mazingira yaliyojengwa sasa jimboni Msalala, ni kama kuwasafishia njia wenzetu wa Chadema kupata ushindi mwaka 2015,” alisema.

Maige alikana kuhusika kuandaa mapokezi akitokea jijini Dar es Salaam baada ya kuvuliwa uwaziri, akasema yalikuwa ya wananchi wa Msalala.

Alisema kwa kipindi cha miaka saba alicholiwakilisha jimbo hilo, hakuwahi kuona umati mkubwa ukihudhuria mkutano wake kama ilivyokuwa wakati wakimpokea.

Akiwa katika mkutano wa hadhara na kufungua matawi kwenye kata ya Makukwe wilaya ya Newala mkoani Mtwara juzi, wakazi wa eneo hilo walimueleza Mnyika kuwepo tuhuma za ufisadi wa watendaji katika halmashauri hiyo ambayo Mbunge wake ni George Mkuchika.

Akijibu hoja hiyo, Mnyika alisema kinachopaswa kufanywa na wananchi wa eneo hilo ni kumuadhibu kwa kutomchagua Mkuchika, kwa vile ameonyesha udhaifu wa uongozi hata akiwa Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa).

Mnyika alisema akiwa Tamisemi, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh ilionyesha kuwepo ufisadi kwenye halmashauri zilizokuwa chini ya Mkuchika aliyeshindwa kuudhibiti.

Mnyika alisema kwa vile Mkuchika ni Mbunge wa Newala, anapaswa kuwatendea haki wakazi wa jimbo hilo kwa kuagiza uchunguzi ufanyike dhidi ya tuhuma hizo na kushinikiza kurejeshwa kwa Sh. bilioni 40 za Kagoda ili zitumike kuboresha kilimo kama cha korosho.

Alisema Mkuchika ana wajibu huo kwa vile Rais Kikwete alishaagiza fedha hizo kuwekwa kwenye Benki ya Uwekezaji (TIB).

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

0 Maoni:

Post a Comment