Tuesday, May 22, 2012

Shibuda atoswe-BAVICHA Arusha

BARAZA la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Arusha limeunga mkono tamko lililotolewa na mwenyekiti wao wa taifa, John Heche, dhidi ya Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda, na kukiomba chama hicho kuchukua maamuzi magumu ya kumtimua mbunge huyo.

Mwenyekiti wa BAVICHA mkoani hapa, Ephata Nanyaro, aliyasema hayo jana alipoongea na waandishi wa habari, na kudai kwamba vijana wamesikitishwa na kauli ya kukidhalilisha chama chao iliyotolewa na Shibuda kwenye mkutano wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alisema kuwa wao hawana tatizo na nia yake ya kugombea urais mwaka 2015 bali wamefadhaishwa na madai kuwa chama pekee kinachoweza kushika dola ni CCM jambo walilosema ni sawa na uhaini.

“Chama chetu kimepita katika mapambano na changamoto mbalimbali. Ni chama pekee ambacho kimewahi kuchukua maamuzi magumu na kubaki imara, katika hili la Shibuda tunaomba chama kichukue maamuzi magumu, hata kwa gharama ya jimbo” alisema Nanyaro ambaye pia ni diwani wa kata Levelosi.

Alisema kuwa CHADEMA imejipanga kuchukua dola kwani ina mfumo mzuri wa kiuongozi kutoka ngazi ya chini hadi taifa na ni chama pekee chenye katiba bora na kinachotetea kwa vitendo maslahi ya umma na ni tumaini pekee kwa mamilioni ya Watanzania.

“Shibuda kutangaza kuwa anataka kugombea urais kupitia CHADEMA mwaka 2015 siyo tatizo. Tatizo ni kukidhalilisha chama mbele ya CCM; ukiwa na askari katika kikosi chako ambaye anaamini majeshi ya adui ni bora zaidi na yanastahili kushinda vita askari huyo anakuwa ni msaliti na anapofanya kazi au jitihada ya kutaka adui ashinde kijeshi huo ni uhaini,” alisema Nanyaro.

Mvutano baina ya Shibuda na BAVICHA uliibuka baada ya mbunge huyo wa Maswa Mashariki (CHADEMA) kutangaza kwamba atagombea urais mwaka 2015 kupitia chama hicho na kumuomba Rais Jakaya Kikwete awe meneja wake wa kampeni wakati wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), mjini Dodoma.

Tayari Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, Heche, amesema kuwa Shibuda ataanza kujadiliwa Alhamisi wiki hii kupitia vikao halali vya baraza hilo na mapendekezo yao yatapelekwa kwenye vikao vya juu vya chama kwa ajili ya maamuzi.

chanzo;Tanzania daima

0 Maoni:

Post a Comment