Tuesday, May 22, 2012

Makundi ya urais bado yaitesa CCM

Sasa Pinda awapiga marufuku MaRC na MaDC
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

Makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yamekuwa ni tatizo kubwa kiasi kwamba sasa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ametoa ilani kwa wakuu wa mikoa na wilaya, kujitenga nayo vinginevyo wataharibikiwa.

Ingawa Pinda hakutaja makundi mahususi, makundi ambayo yanatafunana ndani ya CCM ni yale yanayosaka urais wa mwaka 2015 kupitia chama hicho.

Joto la kusaka urais mwaka 2015 kupitia CCM ni kubwa kiasi kwamba kila uteuzi unaofanywa katika nafasi za kisiasa kama uwaziri, ukuu wa mkoa, ukuu wa wilaya na hata uteuzi wa wabunge wa kuteuliwa, unatazamwa katika sura ya urais mwaka 2015.

Rais Jakaya Kikwete anamaliza ngwe yake ya miaka kumi mwaka 2015 hali inayotoa fursa kwa mwanachama mwingine wa chama hicho kuteuliwa kupambana na wagombea wa vyama vya upinzani.

Baadhi ya wanachama wa CCM ambao wamekuwa wakitajwa kuwa wanausaka urais, ingawa wenyewe wamekuwa ama wakikanusha au kukwepa kuzungumzia kwa undani nia zao ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli kupitia CCM.

Wengine ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

Akitoa maelekezo hayo jana wakati akifungua mafunzo ya siku 10 kwa mawaziri 17, wakuu wa mikoa, na makatibu tawala na wakuu wa wilaya, mjini Dodoma, Pinda aliwataka viongozi hao kujiweka pembeni na makundi hayo na badala yake wakawatumikie wananchi.

Aliwaonya kuwa wasipojitenga na siasa za makundi sasa, kujitoa kwake kutakuwa kugumu baadaye.

“Hili niliseme, lakini I hope (natumaini) mtanielewa, changamoto hii katika kupita pita huko imejitokeza sana, ninyi ni viongozi ambao tumewapa hiyo dhamana…maeneo yenu pia yana siasa, chonde chonde, usitumbukie kwenye siasa hizi za makundi,” alisema na kuongeza:

“Siasa ambazo zinaendeleza mgawanyiko kwenye wilaya yako au kwenye mkoa wako we uko pale kuhakikisha kuwa jamii inatekeleza jukumu la kuleta maendeleo kwa watu, ukitumbukia tu huko tabu, kujitoa inakuwa tatizo kubwa sana stand as a leader (simama kama kiongozi) tekeleza majukumu yako kwa mujibu wa sheria, Katiba yetu, kanuni, you look as a smart guy (utaonekana mtu makini), " alisema.

Alionya kuwa watu wakishaanza kuwasema kuwa wao ni wao itawaletea tabu katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Wakianza kukusema yule mkuu wa mkoa ni wangu, wangu kwa lipi? Kwa hiyo tusimamie, tusimame kidete kabisa kuhakikisha majukumu yetu ya msingi yanaenda vizuri, vinginevyo na nyinyi mtaingizwa katika mgogoro huo huo.

Mkuu wa mkoa huu na yeye anachangia hapa, wako na mbunge fulani, sijui na nini, ukishaingia itakupa tabu na jitahidi ujue namna unavyoweza ku-behave (kujiheshimu),” alisema.

Wakuu wengi wa wilaya na wa mikoa wamekuwa wakiziunga mkono kambi za makundi hayo yanayousaka urais.

Hali hiyo imesababisha baadhi ya wananchi kuuchukulia uteuzi wao kuwa ni fadhila na kwamba wengine wameteuliwa kwa ajili ya makundi mbalimbali ndani ya CCM kujipanga kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

KUJIHESHIMU

Pinda alisema viongozi hao ni kioo katika jamii wanayoiongoza na kuwataka kujiheshimu kwa kuweka mipaka.

“Umealikwa katika eneo fulani kwamba lazima uende pale…unaweza kuwa mtu mzuri sana mnenguaji mzuri, lakini umeshakuwa DC basi,” alisema.

Alisema nafasi nyingine ni nzuri, lakini zinawapa mipaka ambayo ina athari katika uhuru wao binafsi. “Tujiheshimu, kunywa kabia chako ujiheshimu, hata ukitaka kudondoka katika mapungufu ya binadamu dondoka kwa heshima don’t make open kabisa,”alisema.

RUSHWA

Waziri Mkuu alisema mkuu wa wilaya mzuri ni anayeomba msaada kwa viongozi wengine.

Alitolea mfano mkuu wa wilaya anaweza kuomba msaada kwa mkuu wa polisi wa wilaya ili aweze kusaidiwa katika suala la kupambana na rushwa.

“Unafahamu kuwa kuna rushwa nyingi katika halmashauri yako, hapa kuna watu wanajilimbikizia mali, wengine wamejenga majumba, wengine wamenunua magari matatu juzi, wamejilimbikizia fedha ambazo moja kwa moja zinahusiana na fedha za serikali za mitaa wachukulieni hatua,” alisema.

Alisema anajua kuna watu ambao wataona kuwa wakuu wa wilaya ni wafitini ama ni wambeya kwa kulivalia njuga suala la rushwa, lakini wasijali.

UPATIKANAJI WA CHAKULA

Pinda alisema ni aibu kwa mkoa kuomba chakula na kuwataka viongozi hao kuhakikisha kuwa wananchi wanazalisha katika maeneo yao chakula cha kutosha.

Aliipongeza mikoa ya Dodoma na Singida ambayo awali ilikuwa ikiomba omba sana chakula, lakini hivi sasa wamejitahidi kukabiliana na upungufu huo.

Aliwataka kuwashawishi wananchi kulima mazao ambayo yanaendana na hali halisi ya eneo husika ili wazalishe kwa wingi.

UJENZI

Aidha, aliwataka kuangalia mfumo wa upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kwa wananchi ambao utawawezesha wengi kuvipata kwa urahisi.

Alitolea mfano katika jimbo lake ambapo aliandaa mfumo uliowawezesha kupeleka mabati katika eneo hilo na kuyauza yote.

Aliwasisitizia kuwa wakati mwingine siyo kwamba watu wanakuwa hawana fedha, bali ni namna ya upatikanaji wa vifaa hivyo, katika maeneo mbalimbali wamekuwa wakisafiri safari ndefu kutafuta huduma hiyo.

USHIRIKIANO

Aliwataka kuwa kiungo na makundi mengine yote ikiwemo vyama vya siasa, viongozi wa dini na taasisi zisizo za kiserikali na wafanyabiashara.

Aliwataka viongozi hao kuitisha vikao na wafanyabiashara ili wawasaidie katika kusukuma maendeleo ya wilaya zao.

AJIRA KWA VIJANA

Waziri Mkuu alisema wao ndiyo walengwa katika suala zima la kushughulikia tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Alisema fursa za ajira nyingi zipo vijijini na kuwataka kuwapa kipaumbele vijana katika ajira hizo.

MIGOGORO YA ARDHI

Aliwataka kushughulikia migogoro ya ardhi na kutaka utaratibu utakaoshughulikia kutegemea busara, hekima na sheria na ushirikishwaji wa jamii kwa kiasi kikubwa.

“Haya mengine unayoyaona yanaibuka kutokana na hisia zetu za kisiasa, tutaendelea kulisema, lazima tuwaambie Watanzania kuwa tabia inayoanza kujengeka ya watu kutaka kufanya vitu bila kufuata taratibu bila kufuata sheria haikubaliki,” alisema na kuongeza

“Unataka kwenda kuchoma shamba la mtu, shamba ambalo amekabidhiwa kisheria, hili haliwezi kukubalika.”

Pinda alisema ni lazima watu waheshimu sheria, kufuata utaratibu na kuwataka kusimamia kwa karibu sana, vinginevyo wataleta shida na kutisha wawekezaji. Alisema wahalifu lazima wakamatwe na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.

KUWASIKILIZA WANANCHI

Pinda aliwataka kutengeneza taratibu za kuwasikiliza wananchi.

“Naomba niwaombe sana wasikilizeni Watanzania hawa, wapeni fursa waeleze matatizo yao, tengeneza utaratibu, mengine unakuta kweli kuna kuonewa na kazi yenu ni kuhakikisha kuwa hawaonewi bila sababu za msingi,” alisema.

Aliwataka kuacha kukaa ofisini na badala yake kutoka na kwenda kusikiliza matatizo ya wananchi na kisha kuyatatua.

CHANZO: NIPASHE

0 Maoni:

Post a Comment