Wednesday, October 23, 2013

Vyama vyakabidhi mapendekezo sheria ya katiba


Hatimaye vyama vya siasa vilivyo na uwakilishi, kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM) na visivyokuwa na uwakilishi bungeni vimewasilisha serikalini mapendekezo ya kuboresha sheria ya marekebisho ya Sheri ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013.

Msemaji wa vyama hivyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa mapendekezo hayo yalikabidhiwa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

Mbatia, ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa, alisema hayo baada ya vyama hivyo kukutana jana katika kikao chake cha tatu tangu wakutane na Rais Jakaya Kikwete Ikulu, jijini Dar es Salaam, Oktoba 15, mwaka huu.

Kikao hicho cha jana, kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.

Wengine ni Isack Cheyo (aliyemwakilisha Mwenyekiti wa UDP), Nancy Mrindoko (aliyemwakilisha Mwenyekiti TLP), Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa, ambaye aliviwakilisha vyama visivyokuwa na uwakilishi bungeni.

Mbatia alisema kamati ya serikali na ya vyama vya siasa watakutana na kwamba, wamekubaliana mapendekezo hayo yapelekwe katika Mkutano ujao wa Bunge unaotarajiwa kuanza wiki ijayo kwa hati ya dharura.

Mbatia alisema suala hilo litajadiliwa katika mikutano ya wabunge wa vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni.
 
CHANZO: NIPASHE

0 Maoni:

Post a Comment