Tuesday, October 15, 2013

Je ICC inaonea Afrika?

Huku Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akikabiliwa na shinikizo kufika mbele ya mahakama ya kimataifa ya jinai ICC mwezi ujao, kujibu mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu dhidi yake , Muungano wa Afrika umeitisha mkutano maalum kujadili uhusiano wake na mahakama ya ICC.
Muungano wa Afrika wenyewe umekumbwa na mgawanyiko kuhusu mahakama ya ICC, huku viongozi wa Afrika Mashariki wakikabiliwa na upinzani kutoka kwa wenzao wa Afrika Magharibi wanaounga mkono mhakama hiyo.

Hisia ni kali kuhusu mahakama hiyo.Upinzani dhidi ya mahakama hiyo ambayo imekuwepo kwa miaka 11, unatoka zaidi kwa Afrika Mashariki , hasa kwa sababu viongozi wake wawili wanatakikana na mahakama hiyo , Rais wa Sudan Omar al-Bashir na wa Kenya Uhuru Kenyatta. Naibu rais William Ruto tayari yuko mbele ya mahakama hiyo kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu.

Mahakama ya ICC imekuwa kwenye ajenda ya AU tangu makama hiyo kutoa kibali cha kumkamata Rais Bashir na nchi zinazoipinga vikali ni pamoja na Kenya, Sudan na Uganda.
Nchi za Afrika Mgharibi zinazoipinga ni Nigeria, Ghana na Botswana.
Licha ya tetesi kuwa mkutano huo utajadili hatua ya wanachama 34 wa Afrika waliotia saini mkataba wa Roma zijiondoe kwenye mahakama hiyo, waziri wa mambo ya kigeni wa Kenya alisema kuwa haiwezekani kwa viongozi kuungana kujiondoa katika mahakama ya ICC.
Bwana Ruto na Rais Kenyatta ni viongizi wa kwanza wa Afrika kufikishwa mbele ya mahakama hiyo.

Wawili hao wanatuhumiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu. Wadaiwa kupanga na kuongoza ghasia za kikabila zilizozuka baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007-08. Watu zaidi ya elfu moja walipoteza maisha yao na wengine laki sita kuachwa bila makao.
Wote wamekanusha madai hayo na walichaguliwa kama rais na naibu wake wakenya wakipuuza onyo la Marekani la athari kutokea ikiwa wawili hao wangechaguliwa.
Wadadisi wanasema kuwa mahakama ya ICC inaoenekana kama ukoloni mambo leo na kuonea nchi za Afrika.
Pamoja na hilo, serikali ya Afrika Kusini yenye ushawishi katika Muungano wa Afrika, pia ilikosoa mahakama hiyo ya ICC.
Chama tawala cha ANC kilisema hapo nyuma kuwa ICC inataka kufanya mapinduzi nchini Kenya kwa kutumia sheria zake kwa kusisitiza kuwa Kenyatta na Ruto wawe katika mahakama hiyo wakati kesi zao zikiendelea badala ya wao kuwepo wakati kesi hizo zikielekea kumalizika.
Chama hicho kilisema kuwa mahakama ya ICC imekuwa chombo cha kubadilisha uongozi katika nchi za kiafrika. Sio Afrika Kusini pekee bali pia Zimbabwe ambayo imesema kuwa Tony Blair na George Bush wanapaswa kuwa kizimbani kwa kuvamia Iraq.

Kaskazini mwa Afrika ni Tunisia pekee inayounga mkono ICC.

Cha muhimu zaidi, Muungano wa Afrika umekosa kuimarisha uhusiano wake na ICC, tangu mwendesha mkuu wa mashitaka Fatou Bensouda wa Gambia kuchukua usukani mwaka jana kama mwendesha mkuu wa mshitaka.
AU imekosoa sana AU kwa sababu ya kuwashitaki viongozi wa Afrika pekee.

Uganda imekuwa ikisema kuwa mahakama ya ICC inatumiwa na watu wasiokuwa na nia njema na ambao wanajaribu kubadili utawala katika mataifa fulani.
Lakini rais wa Ghana John Mahama ameunga sana mkono ICC akisema kuwa imeweza kuwachukulia hatua wale waliokiuka haki za binadmau na kufanya mauaji bila kujali. Ila alipinga kushitakiwa kwa Uhuru Kenyatta na Naibu wake kwani walichaguliwa kama viongozi.
Licha ya tofauti hizi kati ya ICC na mataifa ya Afrika, wananchi wa Afrika wana msimamo tofauti kabisa kuhusu mahakama hiyo wengi wakiiona kama njia ya pekee kunusuru raia wa Afrika wanaokandamizwa na viongozi wasiojali sheria wala haki za binadamu.
Siku ya Jumatatu mashirika 130 yasio ya kiserikali nchini Kenya yaliandika barua kwa AU yakionya kuwa kujiondoa kwa mataifa ya Afrika katika mkataba wa Roma, kutaonyesha kuwa viongozi wa Afrika hawako tayari kulinda haki za watu pamoja na pia yataonekana kama yanayounga mkono tabia ya watu kukiuka sheria bila ya kujali.

Aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan pia ameyaonya mataifa ya Afrika kutoondoka ICC.

0 Maoni:

Post a Comment