Friday, November 16, 2012

RIPOTI MAALUM: Mtandao wa ufisadi, siri hadharani

 

Miaka michache iliyopita iliibuka kashfa ndani ya chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo kwa kiasi kikubwa ilikitikisa na kukiyumbisha. Kashfa hiyo ilitokana na mkataba ambao ulitiwa sahihi na uongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM na kampuni ya Bwana Subhash Patel kwa mintarafu ya kujenga jengo kubwa kuliko yote hapa Dar es Salaam (kwa sasa) kwa njia ya ubia kwenye kiwanja kilichopo kwenye kona ya barabara za Morogoro na Lumumba.

Ni dhahiri kuwa ufisadi hapa nchini Tanzania ni nadra kujulikana mpaka inapotokea wale wadau wa ufisadi husika wanapokorofishana. Hapo ndipo huwa ‘mambo hadharani'. Vinginevyo, ukitegemea vyombo vya dola ndivyo vianike uoza basi utasubiri milele. Kwani inakisiwa kuwa mara nyingi navyo huhusika kwenye maovu hayo au katika kuyaficha.

Sasa kashfa hii iliibukaje hadharani? Kashkash hii ilianza pale mwanachama wa CCM mwandamizi Bwana Nape Nnauye alipotaka kugombea uenyekiti wa UVCCM yaani Umoja wa Vijana wa CCM Taifa. Majungu yakaanza na jina lake kufutwa na hapo ndipo kisu kikafika mfupani. Nape akatangaza hadharani kuwa kuna ufisadi mkubwa ndani ya UVCCM na ndio maana jina lake limefutwa.

Nape akatema cheche, ‘Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya UVCCM Bwana Edward Lowassa, (Waziri Mkuu aliyejiuzulu kutokana na kashfa nyingine ya ufisadi ya Richmond) pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM (wa wakati ule) Bwana Emmanuel Nchimbi ndio waliosaini mkataba kwa upande wa UVCCM kuingia ubia na Subhash Patel'. Alisema mkataba huo ulisainiwa kinyemela na haukupitishwa na mamlaka halali za UVCCM. Aidha, mkataba huo ulimpendelea mno Subhash na hata kufikia mahali Subhash akabidhiwe jengo la UVCCM ili aliweke dhamana ili akope benki kwa ajili ya ujenzi huo. Yaani ni kisa cha kumkaanga samaki kwa mafuta yake!

Hatimaye, Kamati Kuu ya CCM iliunda ‘tume ya uchunguzi ambayo hadi leo haijulikani iliishia wapi. Bwana Nape alizuiwa kugombea uenyekiti wake na baadae kidogo Mwenyekiti Jakaya Kikwete akamteua kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi kwenye Sekretarieti ya Taifa ya CCM. Cheo kikapanda na mdomo wake ukazibwa, kimya.

Bwana Subhash ni mfanyabiashara mashuhuri hapa Dar es Salaam ambaye mara nyingi amekuwa akijinasibu na kutamba hadharani kuwa yeye ni mzaliwa wa kijiji cha Msoga, Chalinze na kuwa yeye na Rais Jakaya Kikwete tangu utotoni wamekua pamoja hapo kijijini. Utajiri wake wa ghafla Subhash umezua maswali mengi hapa nchini tangu enzi za awamu ya pili. Aidha uhusiano wake na Rais Mwinyi na (madili yake pale Wizara ya Fedha) nayo pia yameacha hisia zenye utata mtupu.

Inasemekana mwaka 2005 Kikwete alipogombea uraisi kwa mara ya kwanza, Subhash kupitia njia mbalimbali aliifadhili kampeni ya Urais kwa kiasi cha mabilioni ya shilingi hadi mwisho. Pamoja na kuwa CCM ilipata ufadhili mkubwa kutoka Uarabuni, Afrika ya Kusini, Kampuni za madini na bila ya kusahau fedha za wizi za EPA kutoka Benki Kuu ya Tanzania, bado Subhash nae alibaki mstari wa mbele kwenye zoezi hilo.

Waingereza wana msemo ‘'A favour begets another'. Yaani anaekufanyia fadhila fulani basi ujue iko siku nae atataka uilipe. Haiwezekani Bwana Subhash akamwaga mapesa yote hayo kwa sababu anampenda sana Rais mtarajiwa. Au kuwa Bwana Subhash ana mtambo wa fedha za kumwaga zisizo na mwisho? La hasha! Yeye na wengine walikuwa wanawekeza ili wapate utajiri usiomithilika hapo baadaye kwa kutumia vibaya jina la Rais kuwatisha watendaji na wafanyabiashara wenzake. Vinginevyo wafadhili wote hao walikuwa na haja ya kulinda ‘madudu na ngawira (loot)' walizokwapua hapa nchini.

Hebu tuchepuke kidogo: Kama sote tujuavyo, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) limekabidhiwa miradi mikubwa na muhimu hapa nchini. Pamoja na miradi mingi, limekuwa likisimamia pia mradi mkubwa wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na mradi wa madini ya chuma wa Liganga iliyopo Ludewa huko kusini ya Tanzania kwa takriban miaka 40 sasa. Kwa shinikizo la 'wakubwa' na kinyume na ushauri mahiri wa kitaalamu mradi huo uligawanywa na kumegwa vipande ili hatimaye akakabidhiwa Bwana Subhash moja ya kipande cha miradi hiyo katikati ya wingu la rushwa.

Ufisadi huu ulizungumzwa kwa kina bungeni mwaka 2006 (hansards za bunge la bajeti la 2006 zahusika). Hata hivyo, juhudi za wanaharakati kuzuia mradi huu ziligonga ukuta kwa kuwa ulufanyika ulaghai kuonyesha Bwana Mkubwa alishinikiza mamlaka zinazohusika zihakikishe mradi huu unakabidhiwa kwa M. M. Steel ambayo ni kampuni ya Subhash. Upo ushahidi unaothibitisha namna ‘jina la Bwana Mkubwa kutumika katika kufuatilia mchakato huo. Ili kuhakikisha zoezi hili halikwami, Waziri Mkuu (sasa mjiuzulu) alihakikisha anateuliwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa NDC ambaye ni wa kabila lake. Wengine waliosaidia ‘gemu' hii ni pamoja na Waziri wa Biashara na Viwanda, aliyejiuzulu baadae kwa kashfa, kwa kuwatisha wahusika hadi mpango huo ulipofanikiwa.

Tukirudi UVCCM, magazeti yakaripoti kwa upana yale yote yaliyojiri kuhusiana na ufisadi wa mkataba wa ubia. Hata hivyo, pamoja na ushahidi wa dhahiri ulioweka wazi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa UVCCM Bwana Lowassa pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM Bwana Nchimbi walihusika moja kwa moja kwa kusaini mkataba mbovu wa kifisadi na Bwana Subash; CCM yenyewe iliogopa kuchukua hatua kwa sababu ambazo watafiti wengi waliziona kuwa ni za kisiasa.

Aidha, uhusiano wa kivuli cha Mwenyekiti Kikwete na Subhash, ambaye kwa kujua ama bila kujua alikuwa na deni la fadhila kwa Subhash, usingeruhusu haki na sheria kufuata mkondo wake. Isitoshe, pamoja na harakati zote za CCM za kushinda uchaguzi wa mwaka 2005, Kikwete aling'amua mapema kuwa Lowassa aliwekeza mno kwenye ‘mtandao ndani ya CCM kiasi kuwa Kikwete asingethubutu kumwajibisha Lowassa kwa ufisadi wa UVCCM. Watazamaji wa kisiasa wanaamini kuwa kwa hivi sasa, Lowassa anamiliki mtaji mkubwa zaidi ndani ya CCM kuliko Kikwete.

Kwa vile sote sasa tunajua maslahi ya Kikwete yaliyotokana na Subhash yamelengwa wapi, hebu tuangalie maslahi ya wachezaji wengine yalipokaa. Maslahi ya Bwana Lowassa hayako dhahiri sana mpaka sasa lakini ukiangalia namna ambavyo anagawa pesa kwa makanisa mbalimbali na Bakwata utapata angalau dalili ya kiasi cha fedha alizotengeneza ndani ya miaka miwili tu ya uwaziri mkuu wake. Tunafahamu kuwa ana biashara zake, lakini je, fedha hizi anazogawa tukizijumlisha zinawiana na kodi anazolipa TRA?

Wengi wetu tunashangaa, vipi Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa nzito ya Richmond bado analipwa marupurupu ya kustaafu. Hivi Lowassa anaweza kufananishwa na Salim, Warioba, Msuya au Sumaye katika utumishi wao? Kama siyo, basi inakuwaje anaejiuzulu kwa hiari, anaemaliza muda wake kwa salama na yule mwenye kashfa wote wanawekwa kundi moja?

La kushangaza zaidi, Lowassa bado ni mbunge, inakuwaje alipwe na Serikali hiyohiyo mishahara miwili? Jamani, sisi wafanyakazi wa kawaida, tunakatwa NSSF kwenye mishahara yetu kila mwezi. Ili tulipwe ‘NSSF yetu sharti ithibitike kuwa hatuna ajira nyingine. Ikiwa bado tumeajiriwa basi hatulipwi. Sasa maisha ya kisiasa ya Lowassa yananikumbusha kisa cha popo na ndege! Kama huu si ufisadi ni nini?

Twende tuone: Je, Waziri wa Biashara na Viwanda wa wakati ule aliyejiuzulu alifaidikaje kwenye ‘mission' hii? Yeye ni mbia katika kampuni ya shughuli za upakuaji wa makontena za bandari ya Dar es Salaam, TICTS. Anashirikiana na Rostam Aziz, mtu ambaye ni rafiki wa damu na Lowassa na kinara wa kampeni ya kumuingiza Kikwete madarakani ambaye hivi sasa yuko mafichoni kufuatia kujiuzulu ubunge baada ya kuandamwa kisiasa. Rostam naye ana kashfa za kutosha zinazomuandama pamoja na zile za wizi wa EPA.

Tumalize ya Waziri wa Biashara na Viwanda: Kwanza utajiri wake wa ghafla, tokea afisa mauzo wa Twiga Cement hadi Ubunge na Uwaziri hautiririki kimaelezo. Aidha fedha ambazo yeye hupoteza katika mahusiano yake na kina mama mashuhuri inafahamika kwa kina. Lakini kwa namna alivyohangaikia miradi ya Subhash hadi ku-risk kwa kukiuka sheria, ni vigumu kutomhusisha na rushwa au ufisadi.

Haya basi kwa kumalizia, hebu tuangalie sakata la UVCCM lilivyoendelea. Bwana Nchimbi, baada ya kutia sahihi yake kwenye mkataba wa jengo la UVCCM alitunukiwa kiwanja kikubwa tu kule Mbezi Beach, eneo ambalo ni mali ya Subhash ambacho ni Kiwanja Na. 936. Kiwanja hicho kinapakana na viwanja Na. 937 cha Jenerali Mstaafu Mboma na Kiwanja Na. 938 cha Mama Kibona. Mboma alikuwa Mkuu wa Majeshi na Mama Kibona ni mke wa aliyekuwa Waziri wa Fedha awamu ya pili, marehenu Steven Kibona. Viwanja vyote hivyo vitatu vilikuwa ni mali ya Subhash.

Zipo sababu kwanini Subhash alimtunukia Mboma kiwanya ambacho baadae Jeshi la Wananchi (JW) lilimjengea nyumba ya kustaafu pamoja ya kuwa zipo nyumba nyingine nyingi tu hapahapa Dar es Salaaam ambazo yeye Jen. Mboma alizijenga na ambazo anamiliki. Inasemekana kuwa Subhash alipata kufanya biashara na Jeshi la Wananchi kwa kutunukiwa tenda kadhaa za ugavi. Itoshe tu kusema utajiri wa Jenerali nao pia unatisha na hauelezeki.

Nae Mama Kibona anaingiaje kwenye sakata hili hadi apewe zawadi ya kiwanja na Bwana Subhash. Kama tulivyonyambua hapo awali, utajiri wa Subhash kwa kiasi kikubwa ulitokana na ‘mishen tawni' zake pale Wizara ya Fedha kipindi cha Rais Mwinyi cha awamu ya pili. Nae marehemu Kibona alikuwa Waziri wa Fedha wakati huo.

Ufisadi kupitia programu kadhaa pale Wizarani mathalan Debt buyback, debt conversion, import support, EPA nk. nk. ziliwatajirisha wafanyabiashara wengi miongoni mwa jamii za kiasia na kabila moja la kaskazini mwa nchi yetu. Wizi, rushwa na ufisadi ukazaa genge la watu wachache ambao walilala maskini na ghafla wakaamka matajiri wa kutupwa. Maafisa wa Serikali pale wizarani na Benki Kuu hali kadhalika wakaneemeka.

Mwisho wa mchezo huu ni maslahi aliyofaidi Bwana Nchimbi! Waingereza wana msemo, ‘'They are no free lunches', yaani hakuna ruzuku au zawadi za bure maishani. Mwishoni lazima ulipie chochote kile unachopokea, kwa njia moja au ingine. Nchimbi kama Jenerali na Mama Kibona, kapewa kiwanja Mbezi Beach baada ya kumwaga wino kwenye mkataba uliogubikwa na ufisadi mkubwa. Na hivi tunavyozungumza, kampuni ya Subhash, Estim Construction Ltd. inaporomosha majengo ya ghorofa kadhaa kwenye kiwanja hicho. Inaonyesha kale kasungura ka UVCCM hakakuwa kadogo kiasi hicho!

Sasa tujiulize sisi wakereketwa, kuna msafi aliyebaki ndani ya CCM? Naam, hili ndio swali la dola milioni moja!

0 Maoni:

Post a Comment