Friday, October 19, 2012

Maaskofu KKKT watoa tamko zito uchomaji wa makanisa Dar


 Send to a friend
Thursday, 18 October 2012 22:37

Boniface Meenana Kelvin Matandiko
MAASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),  wamelaani uharibifu uliofanyika katika makanisa ya Mbagala, Dar es Salaam na kukemea vitendo hivyo viovu.Kauli ya maaskofu hao ilitolewa katika tamko lao lililosainiwa na maaskofu 20 wa kanisa hilo, wakiongozwa na Mkuu wa KKKT ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa.
Kabla ya kutoa tamko hilo, Dk Malasusa aliwaongoza maaskofu hao kutembelea kanisa la KKKT Usharika wa Mbagala ambalo lilichomwa moto na watu wanaodhaniwa kuwa waumini wa dini ya Kiislamu, Oktoba 12 mwaka huu.
Walisema wamelazimika kuonya  uvunjifu huo wa amani uliofanywa kwa mgongo wa uanaharakati wakitahadharisha kuwa, uvumilivu wao usitumike kuvunja sheria za nchi. “Tanzania yenye amani na mshikamano ni tunda la dini zote, makabila yote, itikadi zote za vyama, rangi zote na hali zote za kiuchumi. Hata wasio na dini wanachangia amani ya nchi hii,” linasema tamko hilo.

Maaskofu hao walisema kwa macho na masikio yao, wameendelea kushuhudia vitendo vya uchomaji makanisa huko Zanzibar, Mwanza, Mdaula, Mto wa Mbu, Tunduru, Rufiji, Kigoma na sasa Mbagala. Walisema wakati wote uvumilivu wa Wakristo huenda umetafsiriwa kuwa ni unyonge na woga. “Sisi maaskofu wa KKKT, tumepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za matukio ya uchomaji wa makanisa katika eneo hili la Mbagala.
”Tumekuwa katika mkutano wetu wa Mwaka wa Lutheran Mission Cooperation (LMC) huko Moshi pamoja na vyama vyote vya Kimisionari vya Ulaya na Marekani. Tumelazimika kukatisha mkutano huo kujionea yaliyotokea Mbagala,” lilieleza tamko hilo. Katika tamko hilo maaskofu hao walieleza kuwa dalili za mateso ya kimbari kama ilivyo kwa mateso ya kanisa; zilianza kitambo na hazikushughulikiwa na waliomrithi Baba wa Taifa.“Dalili hizo ni kama madai yasiyo ya kawaida na ya mara kwa mara kwa Serikali inayodaiwa kutokuwa na dini ambayo ni kama, kulazimisha uvaaji wa alama za kidini katika taasisi za umma ili kurahisisha na kuratibisha tofauti za Watanzania,” wameeleza na kuongeza:

“Tunajiuliza likitokea la Mbagala katika shule zetu na vyuo vya umma, watachomwa wangapi na kuuawa wangapi?”Wameendelea kueleza madai na mashinikizo ya uanzishwaji wa mahakama za kidini hapa nchini, mashinikizo ya kidini yanayoingilia mifumo ya kitaaluma na kisheria na mashinikizo ya kidini juu ya mfumo wa uteuzi wa watendaji wa Serikali na katika ofisi za umma ni madai yenye matatizo.
“Tumeshuhudia wizara zetu zikivamiwa mchana kweupe na kushinikiza kuachiwa kwa watuhumiwa wa uhalifu; tumeshuhudia vituo vya polisi vikichomwa moto; mahakama zikilazimishwa kufunga shughuli zake, misikiti ikitekwa, uhai wa viongozi wa dini ukitishiwa hadharani na viongozi wastaafu wakizabwa vibao hadharani kwa sababu zinazoitwa harakati za kidini. Tumefikia kuhoji, watu hawa wavamie nini ndipo hatua zichukuliwe?”Wamehoji  wanataka kichomwe nini ndipo viongozi wenye dhamana ya kulinda mali na uhai washtuke au auawe nani ndipo iaminike kuwa watu hawa ni tishio kwa usalama wa taifa letu.Wamesema wanawasihi  waumini wa dini na Watanzania kwa jumla, wenye wajibu wa kutii na wasiolazimika kutii, kuzingatia kuwa Mwenyezi Mungu analipenda taifa hili na watu wake.
Kamwe hawezi kuliacha liangamie.Mbali na Dk Malasusa maaskofu wengine waliotia saini tamko hilo ni pamoja na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk Martin Shao, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati,  Dk Thomas Laizer  na  Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza.Wengine ni  Askofu wa Dayosisi ya Kusini, Isaya  Mengele,  Askofu wa Dayosisi ya Kusini Kati, Levis Sanga, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Elisa Buberwa, Askofu wa Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Andrew Gulle  na Askofu wa Dayosisi ya Mkoani Mara, Michael Adam. Wengine ni Askofu wa Dayosisi ya Ulanga-Kilombero, Renard Mtenji , Askofu wa Dayosisi ya Konde, Dk Israel-Peter Mwakyolile, Askofu wa Dayosisi ya Kusini Magharibi, Job Mbwilo, Askofu wa Dayosisi ya Iringa, Dk Owdenburg Mdegella na  Askofu wa Dayosisi ya Morogoro, Jacob Ole Mameo.Katika tamko hilo pia wako Askofu wa Dayosisi ya Mbulu, Zebedayo Daudi, Askofu wa Dayosisi ya Meru, Paulo Akyoo, Askofu wa Dayosisi ya Pare, Charles Mjema,  Askofu Mteule wa Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu na Askofu Mteule wa Dayosisi ya Kati, Dk Alex Mkumbo.
Kanisa jingine lachomwa

Wakati maaskofu hao wakitoa tamko hilo, kanisa jingine  limechomwa moto jana baada ya kijana mmoja asiyefahamika  kutumbukiza kaa la moto ndani ya kanisa la Furaha International Gospel Church lililoko Yombo Makangarawe  na kusababisha kuteketea kwa baadhi ya vifaa vya muziki.

Akizungumza na Mwananchi baada ya tukio hilo, Kamanda wa Mkoa wa Temeke, David Misime alisema tukio hilo limetokea kanisa likiwa limefungwa na wachungaji hawakuwapo kanisani hapo.

“Kanisa lina madirisha ya vitundu kwa hiyo yule kijana alipitisha mkono akaweka moto huo kwenye meza iliyokuwa na vifaa vya muziki, huu ni uchunguzi wa awali na chanzo kinadhaniwa kuwa ni hicho,”alisema na kuongeza kuwa  juhudi za majirani zilisaidia baada ya kuvunja mlango wa kanisa hilo na kuingia ndani ambapo walifanikiwa kuuzima moto huo na kwamba, hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa.

“Kwa hiyo tusihukumu moja kwa moja kwamba kanisa limechomwa moto na watu fulani kwa sababu hatujathibitisha, tunafanya uchunguzi ili kubaini ukweli,” alisema Masime.

0 Maoni:

Post a Comment