Saturday, September 29, 2012

Vita dhidi ya Al Shaabab vyapamba Moto


 
Majeshi Kismayo
Hatimaye wanajeshi wa AMISOM wameuteka mji wa Kismayo.
Msemaji wa jeshi la Kenya Kanali Cyrus Oguna aliambia BBC kuwa wanajeshi wa Kenya kwa ushirikiano na wale wa Somalia walianza harakati zao mapema asubuhi ya leo.
Wakati huohuo, majeshi ya Muungano wa Afrika yameanza mashambulizi dhidi ya Al Shabaab kutoka sehemu za ufuo wa bahari na kudhibiti sehemu za mji wa bandarini Kismayo.
Mji huo ndio ngome ya mwisho ya Al Shabaab
Al-Shabab waliutumia mji huo kuingizia silaha zao Somalia na pia kuwatoza wafanyabiashara kodi.
Lakini kundi hilo lenye uhusiano na Al-Qaeda- limeambia BBC kuwa wameweza kukabiliana na majeshi ya AU na kwamba hakua sehemu za mji huo ambazo zimetwaliwa na AU.
Wanajeshi wa Kenya ni sehemu ya majeshi ya Muungano wa Afrika kwa niaba ya rais mpya wa Somalia.
Msemaji wa jeshi la Kenya Kanali Cyrus Oguna amedokezea BBC kwamba sehemu za Kismayo ziko mikononi mwa majeshi ya AMISOM na kwamba zilizosalia zinatarajiwa kutwaliwa hivi karibuni.
Kwenye taarifa ya awali iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa majeshi ya AMISOM, Luteni Generali Andrew Gutti, AMISOM imewataka wenyeji wa mji wa Kismayo kuwa watulivu. Luteni Generali Gutti alisema kuwa nia na lengo la kuupigania mji wa Kismayo, ni kuwakomboa watu wa Kismayo na kuwawezesha kuishi kwa amani na usalama.
Ramani ya Kismayo
Alidokeza kuwa harakati zinaendelea kulenga maeneo ya Al Shabaab mjini humo.
Aidha alsiema kuwa angewataka wapiganaji waliosalia Kismayo kujisalimisha
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baadhi ya wapiganaji wa kundi hilo walio mjini humo, wameelezea nia yao kutaka kujisalimisha. Nayo AMISOM imewahikikishia usalama wao ikiwa wataweza kujisalimisha
Lakini mwandishi wa BBC anasema kuwa Al Shabaab husalimu amri kwa muda wakati wanapokabiliwa na majeshi yenye nguvu kuwaliko.
Ndege za kivita za Kenya zilifanya mashambulizi ya angani mapema wiki hii na kuharibu bohari lenye silaha za wapiganaji hao mjini humo.
Wiki iliyopita, Al Shabaab walijiandaa kuondoka Kismayo na hata kuwahamisha wapiganaji wao pamoja na silaha.
Mji huo wa bandarini ni muhimu kwa Al Shabaab kwani wanautumia kuingizia silaha na pia kuwatoza kodi wenyeji wa mji huo.
Hatua ya wao kupoteza mji huo, itakuwa ni pigo kubwa kwao, lakini wapiganaji hao wa Al Shabaab bado wana uwezo wa kufanya mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Somalia na wale wa Muungano wa Afrika hata katika sahamu ambazo wanajeshi hao wanadhibiti.

0 Maoni:

Post a Comment