Thursday, June 14, 2012

Profesa atoa ‘darasa’ la urani bungeni





WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, jana alitoa “darasa” bungeni kwa mara ya kwanza kuhusiana na utafutaji, na uchimbwaji wa madini ya Urani na akawaondoa hofu wabunge kuwapo kwa athari za madini hayo kwa watu na mazingira kwa kuwa wapo wataalamu hapa nchini.

Profesa Muhongo ambaye ni mtaalamu wa miamba, akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Tundu Lissu (Chadema), ambaye alihoji ni kwanini Serikali inaendelea na mikakati ya uchimbaji wa madini ya urani wakati haina wataalamu wa kutosha huku nchi nyingine zilizoendelea duniani kama Japan zikifunga vinu vyake vya uzalishaji wa umeme kwa kutumia urani kutokana na athari zake.

Akijibu swali hilo, huku akipigiwa makofi na wabunge, Profesa Muhongo alisema sio kweli kuwa mataifa makubwa yote yanafunga vinu vyake vya kuzalisha umeme vinavyotumia urani, bali bado kuna nchi kama ufaransa ambapo asilimia 75 ya umeme ambao unatumika unatokana na nyuklia ya urani.

Alisema nchi zote zinazoongoza kwa uwepo wa madini ya urani kama Kajikistani,Canada, Ustralia na Marekani zinaendelea na miradi ya urani kwa ufanisi mkubwa.

“Katika Afrika nchi zinazoongoza kwa kuwa na akiba kubwa ya urani kama Niger na Malawi pia zinaendelea na miradi ya urani sawa na Kenya ambayo pia ina akiba ya urani na sasa wameanza mkakati wa kuhakikisha wanakuja kuzalisha umeme ambao sehemu yake itauzwa Tanzania,” alisema Profesa Muhongo.

Alisema hakuna haja ya kuwa na hofu na athari za urani kwani kuna nchi zinachimba lakini hazina wataalamu kama waliopo Tanzania na kuzitaja nchi hizo ni kama Malawi.

Awali Mbunge wa Viti maalumu (CCM), Dk Getrude Lwakatare aliuliza swali akitaka kujua, Serikali inachukuwa hatua gani kudhibiti uchimbaji holela wa madini ya urani.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema kwa sasa bado haijafikia hatua ya uchimbaji wa madini ya urani bali shughuli zinazoendelea hivi sasa ni utafiti na uhakiki wa mashapo ili kuthibitisha kuwapo kwa mashapo ya kutosha yanayoweza kuchimbwa kiuchumi na kibiashara.

Alisema Serikali inaendelea kutumia sera, sheria na kanuni za madini zinazosimamia utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji ,usafirishaji na matumizi ya madini ili kuhakikisha kwamba hakuna uchimbaji holela utakaoruhusiwa katika madini hayo.

Alisema kufuatilia kugundulika madini hayo, katika maeneo kadhaa nchini kama Mto Mkuju- Namtumbo Songea na Bahi,Manyoni, Itigi, Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kwa kila atakayeomba leseni ya uchimbaji anaonyesha namna gani atazingatia kanuni za sheria zilizopo na miongozo iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomic (IAEA).


0 Maoni:

Post a Comment