Friday, May 18, 2012

SHIBUDA KUFUKUZWA CHADEMA


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kitaunda kamati maalum ya kushughulikia tuhuma dhidi ya Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda (CHADEMA), ambapo akipatikana na hatia atakabiliwa na adhabu nzito ikiwemo kuvuliwa uanachama.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya chama hicho na kuthibitishwa na mmoja wa maafisa wake waandamizi, zimesema kuwa kamati hiyo inayotarajiwa kukutana wakati wowote kuanzia sasa inaongozwa na mjumbe wa Kamati Kuu, Prof. Abadallah Safari.

Imedaiwa kuwa kamati hiyo maalumu itamhoji Shibuda kabla ya kutoa mapendekezo yake katika kikao cha baraza kuu ambapo kuna habari kuwa litachukua uamuzi mzito na mgumu dhidi ya mbunge huyo, ingawa imedaiwa kuwa naye atakuwa na haki ya kukata rufaa.

Hii itakuwa mara ya pili kwa kamati hiyo kumjadili Shibuda kutokana na kupingana mara kadhaa na msimamo wa CHADEMA katika masuala ya msingi ya sera na itikadi, likiwemo suala la nidhamu.

Hivi karibuni, akiwa mjini Dodoma, Shibuda alikiuka utaratibu wa chama chake na kukidhalilisha hadharani mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM waliokuwa katika semina, akidai kuwa hajaona chama kinachoweza kuongoza nchi zaidi ya chama tawala.

Katika Bunge la bajeti la mwaka jana wakati wabunge wote wa CHADEMA wakipinga na kususia posho, Shibuda alipingana nao ndani na nje ya Bunge, akidai kuwa ilikuwa ni halali yao kupokea posho hizo alizozibandika jina la ‘ujira wa mwina’

Akizungumza na Tanzania Daima, mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Arusha na Mjumbe wa Baraza Kuu, Samson Mwigamba, alisema kuwa kitendo alichokifanya Shibuda hakikubaliki kwa mujibu wa katiba yao, ingawa anaweza kudai ni haki yake ya Kikatiba.

Mwigamba alisema katiba inamtaka kila mwanachama wao kukipigania, kukitetea na kukieneza chama chao kwa lengo la kushika dola.

Hivyo kitendo cha Shibuda kudai kwamba mpaka sasa hajaona chama kinachoweza kushika dola, ni kukiuka katiba jambo ambalo linaweza kumfukuzisha moja kwa moja uanachama.

Kwa mujibu wa katiba ya chama hicho Shibuda alipaswa kupinga mapendekezo hayo ndani ya vikao vya chama ambapo ndipo hoja ilipoamuliwa badala ya kulizungumzia nje wakati ndani alikuwa nao pamoja.

Tanzania Daima ilimtafuta kwa njia ya simu msemaji wa chama hicho, John Mnyika, bila ya mafanikio ambapo simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita muda mrefu bila ya kupokelewa.

Shibuda alikaririwa na vyombo vya habari juzi akieleza kuwa anataka kugombea urais kupitia CHADEMA na kumwomba Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kuwa meneja wake.

Alipotakiwa kufafanua zaidi kauli yake hiyo aliyoitoa wakati akiwasilisha mada kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) mjini Dodoma, Shibuda alisema anataka kuwa Rais wa Watanzania wote hivyo, hata kura za CCM anazihitaji ndiyo maana akatangaza mbele ya jukwaa lao.

Shibuda alisema hakuna mwanachama wa CHADEMA anayeweza kuwa Rais wa nchi hii bila kupata kura za baadhi ya wanachama wa CCM na Watanzania wengine.

“Hata katika hayo majimbo ambayo CHADEMA tumeshinda, hatukupigiwa kura na wanachama wa CHADEMA pekee, bali walikuwepo hadi wa CCM wanaopenda mageuzi.

“Mimi ni Jemedari katika siasa. Ndiyo, nimetangaza mbele ya jukwaa la CCM kwa sababu nahitaji kura zao. Nahitaji kura ya Kikwete na wana CCM wengine, mimi siyo mtu mwoga wa kutangazia vichochoroni Kariakoo,” alisisitiza Shibuda

Habari na Nasra Abdallah

Chanzo:Tanzania daima

0 Maoni:

Post a Comment