Wednesday, May 30, 2012

Uchaguzi mdogo Jimbo la Sumbawanga kitendawili

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Julius Mallaba,

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imesema haiwezi kuitisha uchaguzi mdogo kwa sasa katika Jimbo la Sumbawanga Mjini, mkoani Rukwa, kwa vile kuna kusudio la kutaka kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, uliotengua matokeo ya ubunge wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo (CCM), Aeshy Khalfan Hillary.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Julius Mallaba, alisema kutokana na kusudio hilo, wataitisha uchaguzi huo iwapo Mahakama ya Rufaa itatengua uamuzi huo wa Mahakama Kuu.

“Hatuwezi kufanya uchaguzi (katika Jimbo la Sumbawanga Mjini), Mawasiliano yaliyopo ni kuwa kuna nia ya kukata rufaa Mahakama ya Rufaa, Tunasubiri kama kutakuwa na utenguzi au la,” alisema Mallaba.

Uamuzi wa kutengua matokeo hayo ulitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Bethwell Mmilla, ambaye alisikiliza kesi hiyo.

Kesi hiyo namba 01 ya mwaka 2010 ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Norbert Yamsebo.

Katika uchaguzi huo uliofanyika mwaka juzi, ulikuwa na ushindani mkubwa, ambapo Aeshi alipata kura 17,328 wakati Yamsebo alipata kura 17,132.

Jaji Mmilla alisema alitengua matokeo hayo kutokana na madai ya kuwapo kwa vitendo vya rushwa na vurugu zilizokuwa zikifanywa na wafuasi wa CCM wakati wa kampeni.

CHANZO: NIPASHE

0 Maoni:

Post a Comment