.HOJA BINAFSI JUU YA MWENENDO WA BARAZA LA MITIHANI LA TAIFA UNAVYOATHIRI ELIMU YA TANZANIA
-
[Chini ya Kanuni ya 54(1), (2) na (3)]
Utangulizi
Mheshimiwa Spika, katika dunia ya leo, ili kila mtu aweze kuboresha 
maisha yake ni lazima awe na elimu. Elimu ndiyo inayomwezesha mtu 
kujitambua na kujimiliki yeye mwenyewe kwanza, pia kuzikabili changamoto
 zinazomsonga, kuyatawala na kuyatumia mazingira yanayomzunguka ili 
kuboresha maisha yake. Ndani ya utandawazi, elimu isiyotosheleza, 
tafsiri yake ni umaskini zaidi; wakati elimu zaidi tafsiri yake ni 
maisha bora zaidi.
-
Mheshimiwa Spika, Nelson Mandela, Rais mstaafu wa Afrika Kusini amewahi 
kusisitiza umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya jamii, kwa kusema kuwa;
“........elimu ni injini kubwa ya maendeleo ya mtu. Ni kupitia elimu 
ndipo binti wa mkulima mdogo anaweza kuwa daktari bingwa, kwamba mtoto 
wa kibarua wa mgodini anakuwa Mkuu wa Mgodi, na mtoto wa kibarua wa 
mashambani anakuwa Rais wa taifa kubwa”. (Mandela, 1991).
“Elimu inakuwa na maana sana kama malengo yake yalikuwa ni kuhakikisha 
kuwa kipindi wanafunzi wanamaliza shule, kila mvulana na msichana 
anapaswa kufahamu kwa kiwango gani hajui, na hivyo kuhamasika kujenga 
matamanio ya kutaka kufahamu zaidi muda wote maishani mwake” (William 
Haley, 1901-1987).
-
Mheshimiwa Spika, ili elimu iweze kuleta mabadiliko ya kweli kimaendeleo
 ni lazima iwe elimu bora-ambayo inalenga kumbadilisha mtu na kumwezesha
 kufikiri, kubuni, kujitambua, kuhoji, kudadisi, kupenda kazi, kuwa na 
mwenendo mwema na kuboresha afya na maisha yake binafsi na ya jamii. 
Elimu ni ukombozi iwapo italenga kumpatia mtu uwezo wa kupambana na 
changamato zinazoikabili jamii na taifa kwa ujumla. Elimu inamjenga mtu 
kuwa raia makini na mzalishaji ndani ya nchi yake (Zombwe, 2007)
-
Hata hivyo, pamoja na umuhimu wa michakato ya kufundisha na kujifunza 
katika kuboresha elimu, bado elimu yetu inapimwa na mtihani ambao 
hutumika kama mizania ya kupima kufuzu ngazi fulani ya elimu. Kutokana 
na ukweli huo, ufaulu katika mtihani umekuwa ndio kigezo muhimu cha 
kuvuka ngazi fulani ya elimu kwenda nyingine na au kupata ajira rasmi. 
Kwa kifupi, mitihani katika mazingira yetu, ndiyo inayoamua mustakabali 
wa kiwango cha -maisha atakayoishi mwananchi. Kwa kuzingatia umuhimu wa 
mitihani katika kuamua mustakabali wa maisha ya mwananchi, maelezo ya 
hoja hii yanalenga kuonesha changamoto mbalimbali zinazolikabili Baraza 
la Mitihani la Taifa, na hatimaye kutoa hoja ya kuliomba Bunge liazimie 
kuiagiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za jamii kufanya uchunguzi 
maalumu kwa Baraza la Mitihani la Taifa kuhusu utendaji wake wa kazi na 
kutoa taarifa Bungeni ili Bunge liweze kufanya maamuzi stahiki kwa 
madhumuni kutoa mwongozo wa namna bora ya kushughulikia masuala ya 
mitihani ambayo yana uhusiano wa moja kwa moja na maisha ya watu.
-
Majukumu na Wajibu wa Baraza la Mitihani la Taifa
Mheshimiwa Spika, Baraza la Mitihani la Taifa ni taasisi iliyoanzishwa 
kwa sheria ya Bunge namba 21 ya mwaka 1973. Taasisi hii, pamoja na mambo
 mengine ina mamlaka ya kutunga, kusimamia na kusahihisha mitihani yote 
nchini Tanzania isipokuwa kwa vyuo vikuu.
-
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba Baraza la Mitihani la 
Taifa ni chombo muhimu sana katika kuamua mustakabali wa maendeleo ya 
kielimu au ya kimaisha ya kijana wa kitanzania aliyehitimu ngazi fulani 
ya elimu. Hii ni kwa sababu walau kwa mazingira ya nchi yetu, kipimo cha
 kwamba mtu amefuzu ngazi fulani ya elimu kinatokana na alama ya ufaulu 
wa mtihani mtu huyo aliyopata katika kuhitimu ngazi hiyo ya elimu.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na umuhimu wa mitihani katika kuamua 
mustakabali wa kiwango cha -maisha atakayoishi mtu kutokana na elimu 
aliyoipata, ni dhahiri kwamba mitihani inatakiwa itungwe kwa umakini 
mkubwa kufuatana na mitaala ya elimu inayotumika kwa wakati huo, ilindwe
 na isimamiwe kwa uangalifu mkubwa ili ikidhi mahitaji yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia uzito wa jambo hili, hitilafu yoyote 
katika kutunga, kusimamia na kusahihisha mitihani hiyo, inamwathiri sana
 mtahiniwa mwenyewe na Taifa kwa jumla. Mtahiniwa anaathirika hasa pale 
atakapofutiwa mtihani kwa makosa ambayo hakuyafanya yeye, na vilevile 
taifa linaathirika sana hasa pale udanganyifu katika mitihani 
unapofanyika na hivyo kuwapata wataalamu bandia (wasio na sifa) na hivyo
 kuendelea kulisababishia taifa hasara kubwa. Aidha taifa linapata 
hasara pale mitihani inapofutwa kutokana na udanganyifu na hivyo kuingia
 gharama kubwa katika kurudia mitihani hiyo.
Mheshimiwa Spika, madhara ya kutosimamia na kudhibiti mitihani ipasavyo 
yanawaathiri vilevile wazazi au walezi wa wanafunzi. Hii ni kwa sababu 
adhabu za kufuta matokeo kutokana na kuvuja kwa mitihani au udanganyifu 
katika mitihani zinawasababishia wazazi/walezi msongo wa mawazo juu ya 
mustakabali wa maisha ya watoto wao. Maumivu wanayoyapata wazazi na 
walezi yanatokana hasa na gharama kubwa walizotumia kuwasomesha watoto 
wao ambao ghafla wanafutiwa matokeo yao kwa sababu ya udhaifu wa 
watendaji wa Baraza la Mitihani.
-
-
-
Changamoto zinazolikabili Baraza la Mitihani la Taifa-
1. Kuvuja kwa mitihani
Mheshimiwa Spika, tatizo la kuvuja kwa mitihani hapa nchini ni la muda 
mrefu. Madhara ya kuvuja kwa mitihani hapa chini hali kadhalika ni 
makubwa. Katika historia ya Tanzania, uvujaji mkubwa wa mitihani 
ulitokea -Novemba 1998 wakati wa mtihani wa taifa wa kuhitimu elimu ya 
sekondari ya kawaida (kidato cha nne) na hivyo kusababisha mtihani huo 
kufutwa na kupangwa kufanyika tena Januari 1999. Inakadiriwa kwamba 
gharama zilizotumika kwa kurudia mtihani huo zilikuwa ni Shilingi 
969,651,329/80 (sawa na Dola za Marekani 1,243,142.72), hii ikiwa ni 
tofauti na gharama za mwanzo. -
-
Mheshimiwa Spika, matatizo ya kuvuja kwa mitihani yamesababisha pia 
wanafunzi kufutiwa matokeo yao na hivyo kuwafanya waishi kwa hofu bila 
kujua mustakabali wa maisha yao. Kwa mfano kwa mwaka 2011 peke yake, 
jumla ya wanafunzi 9,736 -wa shule za msingi na wanafunzi 3,303 wa shule
 za sekondari walifutiwa matokeo yao ya mtihani wa Taifa kutokana na 
udanganyifu katika mitihani ambao kimsingi ulitokana na kuvuja kwa 
mitihani. Pamoja na Serikali kutoa msamaha kwa wanafunzi hao lakini 
taifa linakwenda kuingia katika gharama nyingine kubwa ya kwaandalia 
wanafunzi hao mtihani mwingine, gharama ambazo zingeweza kuepukika kama 
mitihani ingekuwa inasimamiwa kwa uaminifu.
-
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya kichocheo cha kuvuja kwa mitihani 
kinatokana na mfumo wetu wa elimu. Mfumo wa elimu tulionao unasisitiza 
zaidi ufaulu wa mtihani wa mwisho kuliko uwezo aliojengewa mwanafunzi wa
 kukabiliana na changamoto za maisha. Hiki kinaweza kuchangia tatizo 
hili kwa kiasi kikubwa kwani kutokana na hali hii, mwanafunzi 
analazimika kutumia mbinu zozote zile ili kuhakikisha kuwa anafaulu 
mtihani wake wa mwisho ambao ndio utakaoamua hatma ya maisha yake. Kwa 
kweli hili ni tatizo kubwa ambalo linatakiwa kufanyiwa tathmini na wadau
 wa elimu kwani linaathiri maendeleo ya elimu nchini. Kuna haja ya 
kuweka utaratibu wa kutathmini uwezo wa mwanafunzi kwa kipindi chote 
awapo shuleni badala ya kukazania mtihani wa mwisho tu. Kuna umuhimu wa 
walimu kuweka msisitizo wa kuelewa zaidi kuliko ufaulu peke yake. Hii 
ingewajengea wanafunzi ari ya kujitahidi kuelewa zaidi wawapo shuleni.
-
2. Ongezeko la Matukio ya Kughushi Vyeti vya Elimu Vinavyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa.
Mheshimiwa Spika, matukio ya kughushi vyeti vya elimu vinavyotolewa na 
Baraza la Mitihani la Taifa ni dosari nyingine inayomomonyoa ubora wa 
elimu hapa nchini. Aidha tatizo la kughushi vyeti vyenye nembo ya Baraza
 la Mitahani la Taifa kunalipotezea Baraza hilo la Mitihani Sifa na 
Mamlaka ya kuendelea kutoa vyeti hivyo kwa kuwa limeshindwa kudhibiti 
mzunguko wa vyeti bandia.
-
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba matukio ya kuvuja kwa mitihani na 
kughushi vyeti vya elimu si tu yanasababisha watu kukosa imani na Baraza
 la Mitihani la Taifa, lakini pia yanashusha kiwango cha ubora wa elimu 
yetu na pia yanashusha hadhi ya mfumo wa elimu hapa nchini. Aidha, 
Serikali inapata hasara kwa kuingia katika gharama zisizo za lazima za 
kurudia mitihani, na kuwalipa wafanyakazi bandia wenye vyeti bandia 
wanaojipatia fedha za walipa kodi kwa njia ya udanganyifu.
-
Mheshimiwa Spika, matukio ya kughushi vyeti yamekuwa yakiongezeka jambo 
linaloashiria kuporomoka vibaya kwa ubora wa elimu ya Tanzania. Kati ya 
mwaka 1990 hadi 2001 kumeripotiwa matukio 583 ya kughushi vyeti vya 
elimu (Tazama Jedwali na.1)
-
Jedwali 1: Matukio ya Kughushi Vyeti vya Elimu Tangu 1990 hadi 2001-
-
MWAKA
MATUKIO YA KUGHUSHI VYETI
1990
25
1991
41
1992
45
1993
11
1994
26
1995
21
1996
34
1997
45
1998
149
1999
32
2000
95
2001
60
-
Chanzo: Hotuba ya Waziri wa Elimu 2002
-
3. Kushuka kwa Viwango vya Ufaulu
Mheshimiwa Spika, kushuka kwa viwango vya ufaulu ni miongoni mwa mambo 
yanayowapa wasiwasi wadau wakubwa wa elimu hasa wanafunzi wenyewe na 
wazazi/walezi na hivyo kutilia shaka mfumo mzima wa utendaji kazi wa 
Baraza la Mitihani la Taifa. -Pia kupungua kwa viwango vya ufaulu na 
badala yake kuongezeka kwa idadi ya wanaoshindwa mtihani kunaliweka 
Taifa katika hali ya hatari ya kutumbukia katika umasikini uliokithiri 
kwani idadi hii ya wanaoshindwa mtihani wengi wao watokosa fursa za 
ajira na hivyo kuwa tegemezi. Kwa mfano, katika mtihani wa taifa wa 
kidato cha nne, mwaka 2011, ni asilimia 9 tu waliopata daraja la I – III
 na asilimia 91 waliambulia daraja la O – IV
-
Mheshimiwa Spika, ongezeko la idadi ya wanaoshindwa mtihani linatia 
shaka kwani haijulikani alama za wanafunzi zinakokotolewa kwa kutumia 
vigezo gani. Aidha haijulikani vilevile kama mwanafunzi anapimwa kwa 
mtihani ule wa taifa peke yake au maendeleo yake ya kitaaluma 
(Countinous Assessment) anapokuwa shuleni yana mchango katika ufaulu 
wake katika mtihani wa Taifa.
-
Mheshimiwa Spika, wasiwasi unazidi kuwa mkubwa pale ambapo kunakuwa na 
idadi kubwa sana ya wanafunzi wanaoshindwa mtihani na Baraza la Mitihani
 kukaa kimya bila hata kushauri nini kifanyike ili kunusuru elimu ya 
Watanzania. Ukimya na usiri wa utendaji kazi wa baraza la mitihani 
unawakosesha wadau wa elimu wakiwemo wanafunzi, walimu na wazazi taarifa
 za msingi ambazo kama wangezipata mapema na kwa usahihi pengine 
wangefanya vizuri zaidi.
-
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya -Baraza la Mitihani la Taifa halitoi 
taarifa muhimu kwa umma -zinazohusu namna mtihani utakavyofanyika ili 
wadau wote wajiandae vema. Jambo hili halina taswira nzuri mbele ya 
jamii kwani linaonesha kwamba Baraza la Mitihani linawavizia wanafunzi 
ili washindwe mtihani. Kwa mfano Baraza la Mitihani la Taifa halikutoa 
taarifa kwa umma kwamba -lingebadili mfumo wa utahini kwa wanafunzi wa 
darasa la saba ambao wangefanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi wa 
Septemba, 2012.(Mfumo mpya ulikuwa ni maswali ya kuchagua na mwanafunzi 
alitakiwa kutia kivuli (shading) katika jibu sahihi. Na hii ilikuwa ni 
kwa maswali yote -ya mitihani ikiwemo na hisabati). Matokeo ya kutotoa 
taarifa hizo mapema ni kwamba kuna uwezekano mkubwa sana wa wanafunzi wa
 darasa la saba kushindwa mtihani huo si kwa sababu hawana uwezo 
kiakili, bali ni kwa sababu ya mfumo mpya wa utahini ambao hawajauzoea. 
Tayari matokeo ya mtihani wa darasa la saba uliofanyika Septemba, 2012 
yameshatoka na yanadhihirisha maelezo niliyoyatoa hapo juu.
-
-Mheshimiwa Spika, Jambo la kusikitisha ni kwamba licha ya kelele nyingi
 tunazopiga kuhusu tabia hii mbovu ya Serikali ya CCM ikishirikiana na 
Baraza la mitihani kuwafaulisha wanafunzi ambao wamefeli mtihani bado 
imeendelea kuwa kiziwi na kuendelea na mchezo huo mbaya wa kuiangamiza 
elimu ya Tanzania. Kwa mfano katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba
 2012, karibu asilimia 70 ya watahiniwa walishindwa kupata alama 100 
kati ya alama 250 (ambayo ndio ilikuwa alama ya juu kabisa). Matokeo ya 
wanafunzi wengi kushindwa mtihani huo (massive failure) baadhi ya 
sekondari zilikosa wanafunzi kwa kuwa hawakutimiza vigezo vya kuingia 
sekondari. Jambo hili lilipelekea Serikali kutoa agizo la kushusha 
wastani wa ufaulu kutoka alama 100 hadi alama 70 kati ya alma 250 ili 
kujaza wanafunzi katika sekondari ambazo awali zilikosa wanafunzi.
-
Mheshimiwa Spika, huku ni kuwaibia wazazi fedha za michango katika shule
 mbalimbali kwa kuwa ni dhahiri uwezekano wa wanafunzi waliofaulishwa 
kwa njia za ujanjaujanja namna hii hawataweza kuvuka kidato cha pili. 
Aidha hiki ni kitendo kiovu, hakina tofauti na mwanafunzi aliyeiba 
mtihani ili afaulu. Sasa kama Serikali nayo inaiba mitihani ili 
wanafunzi wake wafaulu, kuna haja gani ya kuwa na mitihani?
-
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika katika matokeo ya mitihani ya Mock ya 
kidato cha pili mwaka 2012, katika kanda mbalimbali hapa nchini 
yanaonesha kuwa wanafunzi wengi hawakufanya vizuri. Ila jambo la 
kushangaza ni kwamba katika mtihani wa Taifa wamefaulu vizuri sana. Hii 
inatia shaka kwa kuwa hakuna uwiano wa ufaulu kati ya mtihani wa Mock na
 mtihani wa Taifa. Jambo la ajabu hapa pia ni kwamba mtihani wa kidato 
cha pili mwaka 2012, umeratibiwa na wizara ya elimu badala ya baraza la 
Mitihani. Swali hapa ni kwamba: Ni kwanini mtihani wa kidato cha pili 
usimamiwe na wizara wakati una lengo/kusudio moja sawa na mitihani 
mingine inayoratibiwa na baraza la mitihani?
-
4. Kufaulu Mitihani ya Baraza la Mitihani bila Kujua Kusoma na Kuandika
Mheshimiwa Spika, maajabu ya kufaulu mtihani bila kujua kusoma na 
kuandika ni kashfa na aibu kubwa iliyolikumba baraza la Mitihani la 
Taifa hivi karibuni. Kwa mujibu wa Taarifa ya Haki – Elimu ya Aprili 
2012, ni kwamba wanafunzi 5,200 waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na 
kidato cha kwanza mwaka 2012, hawajui kusoma wala kuandika. Hili ni 
jambo la ajabu kabisa na Tanzania inastahili kabisa kuingia kwenye 
Kitabu cha Kumbukumbu za Maajabu ya Dunia (The Guiness Book of Records) 
kwa kushika nafasi ya kwanza kwa kufaulisha wanafunzi wasiojua kusoma 
wala kuandika. Hii ni kashfa kubwa na Baraza la Mitihani la Taifa 
haliwezi kukwepa kuhusishwa na kashfa hii. Tukio hili, licha ya kuhujumu
 ubora wa elimu ya Tanzania lakini pia limelipotezea Baraza la Mitihani 
la Taifa sifa na mamlaka ya kiuadilifu (moral authority) ya kuendelea 
kusimamia mchakato wa mitihani ya taifa.
-
5. Baraza la Mitihani la Taifa Kutunga Mitihani bila Kuzingatia Mwongozo wa Mtaala.
Mheshimiwa Spika, mtaala wa sasa unatoa mwongozo kwamba mwanafunzi 
afundishwe ili awe na uwezo wa kutenda/kufanya jambo kutokana na somo 
alilofundishwa (competence based curriculum). Hii ina maana kwamba, 
mtihani utakaotungwa kwa mujibu wa mtaala huu unatakiwa kupima uwezo wa 
mwanafunzi wa kutenda/kufanya jambo ambalo atakuwa amejifunza darasani. 
Tofauti ya mtaala wa zamani ni kwamba ulikuwa umejikita zaidi katika 
maudhui ya somo (content based curriculum)
-
Mheshimiwa Spika, Mgogoro uliobainika kati ya mitaala na Baraza la 
Mitihani ni kwamba baraza la mitihani limetunga mtihani kwa kutumia 
mtaala wa zamani bila kutoa taarifa kwa umma na kwa wadau wote wa elimu.
 Hii imeonekana wazi katika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi ambapo 
maswali yote katika masomo yote yalikuwa ni ya kuchagua. Maswali ya 
kuchagua majibu (multiple choice) hayana tatizo kama yatatumika kupima 
ngazi ya kwanza kabisa katika kujifunza.
-
Mheshimiwa Spika, licha ya kuwa maswali ya kuchagua yana umuhumu katika 
kupima uwezo wa wanafunzi kukumbuka mada walizofundishwa darasana lakini
 pia aina hii ya maswali ina hasara zake kama ifuatavyo:
i. Maswali haya hayampatii nafasi mwanafunzi kujieleza ili kuweza kupima uwezo halisi wa mwanafunzi katika kufikiri na ubunifu.-
ii. Si kweli kwamba mada nzima inaweza kueleweka kwa jibu moja tena moja
 tu sahihi. Mfano mzuri katika hili ni masomo ya kijamii (social 
studies) ambayo majibu yake hutegemea mazingira na maoni ya mtu.-
iii. Tatizo jingine ni kwamba maswali ya kuchagua hasa kwa shule za 
msingi ni kwamba hata kama mwanafunzi hajui jibu sahihi, kitendo cha 
kuchagua majibu bado kinampa asilimia 20 ya kuchagua jibu sahihi.
iv. Maswali ya kuchagua hayampi fursa mwalimu au mtoa mtihani kujua 
tofauti kati ya wanafunzi wenye uelewa mkubwa na wale wenye uelewa 
mdogo. Ni muhimu kutambua kwamba njia nzuri ya kuongeza ubora wa mtihani
 ni kutunga maswali yanyopima ngazi mbalimbali za uelewa. Mtihani mzuri 
kwa maana hiyo ni ule unaoanza na maswali rahisi (ya kuchagua) kupima 
uelewa mdogo na kuendelea na maswali magumu kupima uelewa mkubwa.
-
6. Mapungufu ya Sheria ya Baraza la Mitihani la Taifa ya 1973
Mheshimiwa Spika, sheria hii ya Baraza la Mitihani la Taifa, licha ya 
nia yake njema, ni kwamba imepitwa na wakati. Ni wazi kwamba mazingira 
yetu na mahitaji ya elimu ya mwaka 1973 hayawezi kwa namna yoyote ile 
kufanana na mazingira na mahitaji ya elimu nchini kwa sasa. Toka mwaka 
1973 hadi sasa ni kipindi cha takribani miaka 40. Katika kipindi hiki 
kuna mabadiliko mengi yametokea hapa yakiwemo mabadilko katika idadi ya 
wanafunzi, shule, na mitaala, nchini ambayo yanahitaji mabadiliko 
vilevile ya mfumo wa elimu, mitihani na sheria yenyewe inayotoa mwongozo
 wa mambo hayo. Ni rai yangu kwamba ili kuliboresha baraza la mitihani 
la taifa, basi ingekuwa ni busara kutazama upya vile vile Sheria hiyo 
ili kuona kama inakidhi mahitaji ya sasa.
-
7. Kukosekana kwa Chombo Huru cha Kushughulikia Rufaa za Mitihani
Mheshimiwa Spika, wasiwasi mwingine uliotanda miongoni mwa wadau wa 
elimu hasa wanafunzi na wazazi/walezi ni juu ya kutokuwepo kwa chombo 
huru kinachoshughulikia rufaa za mitihani ya wanafunzi. Hali hii inaleta
 mashaka kama haki itatendeka kwa wanaoomba rufaa ili mitihani yao 
isahihishwe upya kutokana na kutoamini kwamba kushindwa kwao mtihani 
uliotangulia kulikuwa halali.
-
Mheshimiwa Spika, imani ya haki kutendeka inakosekana kwa sababu katika 
rufaa hii, mlalamikiwa ni Baraza la Mitihani, anayepokea rufaa ni Baraza
 la Mitihani, na anayetoa hukumu ya Rufaa ni Baraza la Mitihani. Kwa 
kutumia akili ndogo tu ni kwamba Baraza la Mitihani ni lazima litetee 
uamuzi wake wa awali na kwa maana hiyo mlalamikaji ana hatari kubwa ya 
kutopata haki yake. Mfano kidogo hapa ni kwamba katika jumla ya 
wanafunzi wote wa kidato cha nne na sita waliokata rufaa mwaka 2011, 
matokeo ya rufaa yalikazia matokeo ya awali. Vivile hakuna sababu 
iliyotolewa kwamba ni kwanini alama hazikubadilika kwa hata mmoja.
-
Mheshimiwa Spika, Angalizo: Rufani ya Matokeo ya Islamic Knowledge ya 
kidato cha sita 2012, isitumike kama kigezo kwamba Baraza la Mitihani 
linatenda haki sana katika rufani za mitihani kwa sababu rufani hii 
ilikuwa na msukumo au shinikizo la Taasisi za dini na pia kulikuwa na 
tishio la maandamano juu suala hili, kwa hiyo, Baraza lilikuwa katika 
mbinyo mkali na pia Serikali kupitia Wizara ya Elimu iliingilia kati 
katika kusukuma rufani hiyo kushughulikiwa mapema ili kunusuru vurugu 
ambazo zingeweza kutokea endapo maandamano yangefanyika.
-
8. Makosa katika Ukokotoaji wa Alama (Marks) za Watahiniwa
Mheshimiwa Spika, tatizo jingine katika Baraza la Mitihani la Taifa, ni 
makosa katika ukokotoaji wa alama za watahiniwa baada ya kusahihisha 
mitihani hiyo. Mfano mzuri hapa ni makosa ya ukokotoaji wa alama 
yaliyofanyika katika mtihani wa kidato cha sita katika -somo la Islamic 
Knowledge mwaka 2012. Makosa haya yalifahamika kwa kuwa yalikumba kundi 
kubwa la watahiniwa ambao walilamika na kuweka shinikizo la kuchunguza 
jambo hilo. Hii ina maana kwamba kuna uwezekano wa watahiniwa wachache 
ambao ukokotoaji wa alama zao hukosewa, na kwa kuwa hawaleti malalamiko 
alama zao hubaki vilevile kimakosa. Makosa kama hayo huathiri alama ya 
mtahiniwa na hivyo huathiri pia mustakabali wa maendeleo ya mtahiniwa 
huyo kielimu na hata kimaisha.
-
9. Baraza la Mitihani kutokuwa na Ofisi katika kanda za Elimu au Mikoani
Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba kitendo cha Baraza la mitihani kuwa na 
ofisi Dar es Salaam pekee, kushughulikia masuala yote ya mitihani nchi 
nzima ni changamoto ambayo bila mashaka yoyote inaweza kuathiri utendaji
 mzuri wa kazi na ufanisi wa Baraza la Mitihani.
-
Mheshimiwa Spika, kutokuwepo na ofisi za Baraza la Mitihani katika kanda
 za elimu au mikoani kwa vyovyote vile kunaleta ugumu katika upatikana 
wa habari muhimu kuhusu mambo ya mitihani. Aidha ni adha kubwa kwa wadau
 wa elimu wenye matatizo yanayohitaji majibu ya Baraza la Mitihani la 
Taifa kufunga safari kutoka mikoani had Dar es Salaam kupata ufumbuzi wa
 matatizo yao. Hivyo ni rai yangu kwa Serikali, kutazama jambo hili na 
kujenga ofisi za baraza la mitihani mikoani kupunguza mrundikano wa 
mashauri ya mitihani katika ofisi moja ya Dar es Salaam ili kuleta 
ufanisi wa kazi za Baraza la Mitihani la Taifa.
-
Mheshimiwa Spika,
KWA KUWA Baraza la Mitihani la Taifa ni chombo kilichopewa mamlaka kwa 
mujibu wa sheria kutunga, kusimamia na kusahihisha mitihani yote katika 
Tanzania isipkuwa kwa vyuo vikuu;
-
NA KWA KUWA ngazi ya elimu anayofuzu mhitimu inapimwa kwa mtihani wa mwisho wa kuhitimu elimu hiyo;
-
NA KWA KUWA kumekuwa na matukio ya kuvuja kwa mitihani jambo ambalo 
linaathiri moja kwa moja ubora wa elimu ya mhitimu na kuliingizia taifa 
hasara kwa gharama zinazotumika kurudia mitihani iliyofutwa kutokana na 
kuvuja;
-
NA KWA KUWA kumekuwa na matukio ya kughushi vyeti vinavyotolewa na 
Baraza la Mitihani la Taifa jambo ambalo limewapotezea wadau wa elimu 
imani na baraza hilo kwa kushindwa kudhibiti hali hiyo;
-
NA KWA KUWA viwango vya ufaulu vinazidi kupungua huku baraza la mitihani
 likishindwa kueleza kiini cha anguko hilo na kutoa ushauri kwa serikali
 ili kuondoa hali hiyo;
-
NA KWA KUWA kumekuwa na tukio la ajabu la wanafunzi 5,200 kufaulu 
mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi uliosimamiwa na Baraza la Mitihani 
la Taifa bila kujua kusoma na kundika jambo ambalo limeshusha hadhi ya 
baraza la mitihani na kudhalilisha mfumo wa elimu wa Tanzania;
-
NA KWA KUWA wanafunzi wanaokata rufaa za mitihani wanakosa haki yao ya 
msingi ya kutendewa haki katika rufaa hivyo kutokana na kutokuwa na 
chombo kingine kinachoshughulikia rufaa za mitihani;
-
NA KWA KUWA kumekuwa na makosa ya ukokotoaji wa alama za watahiniwa 
jambo ambalo linaathiri maendeleo ya kielimu na ya kimaisha kwa wa 
wahitimu;
-
NA KWA KUWA utaratibu wa kukokotoa alama ya mwisho (final grade) ya 
mwanafunzi hauko wazi na hivyo kumnyima mwanafunzi haki ya kujua alama 
yake imetokana na mchanganuo upi wa kazi/mitihani aliyofanya; kwa mfano 
makosa yaliyofanyika wakati wa ukokotoaji wa matokeo ya mtihani wa 
“Islamic Knowledge” wa kidato cha sita 2012 na Serikali kukiri makosa 
hayo kufanyika;
-
NA KWA KUWA sheria ya baraza la mitihani ya mwaka 1973 inaonekana kutokidhi mahitaji kwa mazingira ya sasa;
-
NA KWA KUWA mtihani wa mwisho (wa taifa) kwa darasa la saba, kidato cha 
nne na kidato cha sita unalenga kuchuja wanafunzi watakaoendelea na 
masomo ya juu na watakaostahili kupata fursa mbalimbali za ajira na 
hivyo kujenga matabaka miongoni mwa wananchi;
-
NA KWA KUWA kutokana na ukubwa wa nchi ya Tanzania, na kuongezeka kwa 
idadi ya watahiniwa baraza linashindwa kusimamia mitihani kikamilifu 
katika maeneo yote jambo ambalo husababisha udanganyifu wa mitihani 
katika baadhi ya maeneo;
-
HIVYO BASI, naliomba Bunge lako tukufu liazimie,
1. Kuiagiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kufanya 
uchunguzi maalumu kwa Baraza la Mitihani la Taifa -kwa kuzingatia hadidu
 za rejea zifuatazo:
-
i. Mfumo wa utendaji kazi wa Baraza la Mitiahani la Taifa.-
ii. Mchakato wa utungaji, usambazaji na usimamizi wa mitihani.
iii. Mfumo wa usahihishaji na ukokotoaji wa matokeo ya watahiniwa.
iv. Mchakato wa kupokea na kushughulikia rufani za mitihani.
v. Uhusiano kati ya Baraza la Mitihani, Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
vi. Uwazi na uwajibikaji wa watendaji wa Baraza la Mitihani
vii. Mfumo wa utoaji habari kwa wadau wa elimu kuhusu mabadiliko au mambo ya msingi ya kuzingatia kuhusu mitihani.
viii. Uwezo wa Baraza la Mitihani -kumudu kazi zake za msingi za 
kutunga, kusambaza, kusimamia, kusahihisha na kutoa matokeo sahihi kwa 
watahiniwa.
ix. Kupitia upya sheria ya Baraza la Mitihani ili kuona kama inakidhi mahitaji ya Baraza la Mitihani katika mazingira ya sasa.
x. Kutoa mapendekezo kwa Bunge juu ya namna bora ya kushughulikia 
masuala ya mitihani ili ikidhi malengo yaliyokusudiwa, na pia kutoa 
ushauri juu ya muundo wa chombo kitakachokuwa kinashughulikia mambo ya 
mitihani.
-
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja.
-
-
______________________________  _____
JOSHUA SAMWEL NASSARI (MB)
MBUNGE WA ARUMERU MASHARIKI
0 Maoni:
Post a Comment