Rais Jakaya Kikwete akiwa na mke wake Mama Salma, wakitoa heshima ya mwisho kwa mwili wa Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Marehemu Bob Makani, kwenye viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam jana.
Viongozi mbalimbali wa kitaifa wa vyama vya siasa na serikali jana waliungana na wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuaga mwili wa mmoja wa waasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Nyange Makani (76).
Bob Makani alifariki Jumamosi usiku katika Hospitali ya Aga Khan kwa ugonjwa wa moyo na kibofu cha mkojo.
Utoaji wa heshima za mwisho katika ukumbi wa Karimjee ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais Jakaya Kikwete; Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal; Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Mawaziri Wakuu Wastaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, Joseph Warioba na Frederick Sumaye.
Wengine ni Mwenyekiti Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe; Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama; Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli; Mke wa Rais Mstaafu, Anna Mkapa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
Wengine ni Mwenyekiti wa Chama cha United Democratic (UDP), John Cheyo; Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Natu Mwamba.
Ibada ya kumsomea dua iliongozwa na Sheikh Maulid Mussa kutoka Msikiti wa Msasani, ambaye alisema kuwa katika maisha ya duniani wanadamu wanapaswa kutomsahau Mungu.
KIKWETE: MAKANI ALILETA MAENDELEO
Akizungumza katika shughuli hiyo, Rais Kikwete, alisema alipopata taarifa ya kifo cha Makani alishtushwa sana, akamtafuta Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freema Mbowe, ili kupata undani wa taarifa hiyo ya msiba, lakini hakumpata.
Alisema Makani katika uhai wake alileta maendeleo makubwa ya kiuchuni na kisiasa kwa kushiriki kuanzisha Chadema, hivyo atakumbukwa kwa mchango wake huo mkubwa.
MBOWE: WATU MASHUHURI WAKUMBUKWE
Kwa upande wake, Mbowe, alisema kuna haja katika Katiba ijayo kuweka kipengele cha kuwakumbuka watu mashuhuri walioiletea sifa nchi kama Bob Makani.
Mbowe alisema Chadema kitamkumbuka Makani kwa mazuri aliyofanya ndani ya chama hicho.
Alisema anamfahamu sana marehemu Makani kwa kufanya naye kazi kwa miaka 21 na kukaa naye kama jirani kwa miaka 15 eneo la Mbezi Beach, na kusema amejifunza mengi kutoka kwa Makani.
“Tulipata taarifa za msiba tukiwa Ruangwa, mkoani Lindi saa nne na nusu usiku, tulishtuka sana, tukaamua kufanya kikao cha ghafla mpaka saa saba usiku na kuamua kusitisha shughuli zote za kichama, turudi Dar es Salaam,” alisema Mbowe.
WASIFU WAKE
Akisoma wasifu wa marehemu, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema, marehemu alizaliwa mwaka 1936 katika Hospitali ya Korandoto Shinyanga na alisoma Shule ya Msingi Ibadakuli SDA baadaye kujiunga na Shule ya sekondari Tabora.
Alisema Makani alijiunga na masomo ya chuo kikuu nchini Uingereza mwaka 1961 na kuhitimu Shahada ya Sheria mwaka 1965, na alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chadena 1998, na kadi ya uanachama ilikuwa namba tatu baada ya Edwin Mtei aliyekuwa namba moja na Brown Ngwilulupi aliyekuwa na kadi namba mbili.
SALAMU ZA OFISI YA AG
George Masaj ambaye pia ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali akitoa salama za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, alisema kumpoteza Bob Makani ni pengo kubwa kwa familia na taifa kwa ujumla na kwamba atakumbukwa kwa mazuri aliyofanya na ni mfano mzuri wa kuigwa.
SALAMU ZA BoT
Naye Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Mwamba, alisema marehemu Makani aliteuliwa kuwa Meneja wa idara ya udhibiti wa fedha za kigeni Septemba Mosi, 1963 na alitumikia BoT kwa miaka 12.
Aliongeza kuwa Makani alikuwa mchapakazi hodari hasa katika kipindi ambacho BoT ilipoungua mwaka 1984.
SALAMU ZA CCM
Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alisema Makani alikuwa ni mtu asiyependa kuongea sana, bali alikuwa mchapakazi hodari na anapaswa kuigwa kwa mazuri aliyoyaacha.
Alisema Makani ni miongoni mwa waasisi wa Chadema, hivyo anapaswa kupongezwa kwa kuleta chachu ya siasa nchini.
SALAMU ZA UPINZANI
Akizungumza kwa niaba ya vyama vya upinzani. Prof. Ibrahim Lipumba, alisema Makani alikuwa ni mtu wa watu na aliyependa mabadiliko.
SALAMU ZA WANASHERIA
Francis Stolla, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisema kifo cha Makani ni pengo kubwa siyo kwa chama tu bali kwa watu wote waliomfahamu.
Alisema Makani alijiunga na TLS mwaka 1986 na kupewa kadi ya uanachama namba 136 kama namba yake ya usajili wa kuwa wakili.
KUZIKWA KESHO
Chadema kitawakilishwa na viongozi wake wa juu katika mazishi hayo wakiwemo Mbowe; Dk. Slaa; Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa Mhamed; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Hamad Mussa Yusuph na Naibu Katibu Mkuu Bara, Zitto Kabwe.
Mwili wa Marehemu Bob Makani unatarajiwa kusafirishwa leo kuelekea Shinyanga Mjini, na Shughuli za kuaga mwili zitafanyika katika viwanja vya Shy-Com kuanzia saa sita mchana na maziko yatafanyika katika kijiji cha Negezi kesho.
0 Maoni:
Post a Comment