WAKILI na Ofisa wa Ufuatiliaji na Ukiukwaji wa Haki za Binadamu kutoka Kituo cha Haki za Binadamu nchini (LHRC), Leticia Ntagazwa, ameshauri Katiba mpya iipe nguvu Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora mamlaka ya kumchunguza rais ili kuepuka ukiukwaji wa haki za binadamu unaoweza kufanywa na kiongozi huyo.
Ntagazwa alitoa ushauri huo juzi alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waangalizi wa haki za binadamu wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini yanayofanyika jijini Mbeya.
Alisema katika mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya, ni vema tume hiyo ipewe meno ya kumchunguza rais, ili kumbana pamoja na serikali anayoiongoza, ili wasikiuke haki za binadamu.
“Tunataka tume hii ipewe nguvu ya kutekeleza maamuzi yake kisheria badala ya kuishia kutoa mapendekezo tu ambayo wakati mwingine hayafanyiwi kazi na serikali,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa katiba ya sasa, Rais wa Jamhuri ya Muungano anaweza kutoa maamuzi ambayo yanakiuka haki za binadamu na hakuna chombo chochote kinachoweza kumchunguza wala kumkemea.
Alifafanua kuwa hali hiyo ni hatari kwa mustakabari wa haki za binadamu ikiwa atajitokeza rais mwenye maamuzi kandamizi kwa haki za binadamu.
Aidha, alishauri tume hiyo kuwa huru na yenye ofisi huru katika kila wilaya nchini badala ya ilivyo hivi sasa ambapo ina ofisi nne tu nchini.
0 Maoni:
Post a Comment